\id 2TI - Biblica® Open Kiswahili Contemporary Scriptures (Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu) \usfm 3.0 \ide UTF-8 \h 2 Timotheo \toc1 2 Timotheo \toc2 2 Timotheo \toc3 2Tim \mt1 2 Timotheo \c 1 \s1 Salamu \po \v 1 Paulo mtume wa Al-Masihi Isa kwa mapenzi ya Mungu, kulingana na ile ahadi ya uzima ulio ndani ya Al-Masihi Isa. \po \v 2 Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. \po Neema, rehema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba\f + \fr 1:2 \fr*\ft Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.\ft*\f* Mwenyezi, na kwa Al-Masihi Isa, Bwana wetu. \s1 Shukrani na kutiwa moyo \p \v 3 Ninamshukuru Mungu, ninayemtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya baba zangu, ninapokukumbuka usiku na mchana katika maombi yangu. \v 4 Nikiyakumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona ili nipate kujawa na furaha. \v 5 Nimekuwa nikiikumbuka imani yako ya kweli, waliokuwa nayo bibi yako Loisi na mama yako Eunike, na ninasadiki sasa wewe pia unayo. \p \v 6 Kwa sababu hii nakukumbusha uchochee ile karama ya Mungu iliyowekwa ndani yako nilipokuwekea mikono yangu. \v 7 Maana Mungu hakutupatia roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi. \p \v 8 Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu, \v 9 ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema, bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Al-Masihi Isa tangu milele. \v 10 Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Al-Masihi Isa, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kupitia kwa Injili. \v 11 Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii. \v 12 Hii ndiyo sababu ninateseka namna hii, lakini sioni haya kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kuwa anaweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hadi siku ile. \p \v 13 Shika kwa uthabiti kielelezo cha mafundisho yenye uzima uliyoyasikia kwangu, pamoja na imani na upendo katika Al-Masihi Isa. \v 14 Ilinde ile amana uliyokabidhiwa kwa Roho wa Mungu akaaye ndani yetu. \p \v 15 Unajua ya kuwa watu wote katika jimbo la Asia wameniacha, miongoni mwao wamo Filego na Hermogene. \p \v 16 Bwana Isa akawahurumie watu wa nyumbani mwa Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha mara kwa mara, wala hakuionea aibu minyororo yangu. \v 17 Badala yake, alipokuwa Rumi alinitafuta kwa bidii hadi akanipata. \v 18 Bwana Isa na amjalie kupata rehema zake siku ile! Nawe unajua vyema jinsi alivyonisaidia huko Efeso. \c 2 \s1 Askari mwema wa Al-Masihi Isa \p \v 1 Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo ndani ya Al-Masihi Isa. \v 2 Nayo mambo yale uliyonisikia nikiyasema mbele ya mashahidi wengi, uwakabidhi watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha watu wengine vilevile. \v 3 Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Al-Masihi Isa. \v 4 Hakuna askari yeyote ambaye akiwa vitani hujishughulisha na mambo ya kawaida ya maisha haya kwa sababu nia yake ni kumpendeza yule aliyemwandika awe askari. \v 5 Vivyo hivyo, mwanariadha hawezi kupewa tuzo ya ushindi asiposhindana kulingana na kanuni za mashindano. \v 6 Mkulima mwenye bidii ya kazi ndiye anayestahili kuwa wa kwanza kupata fungu la mavuno. \v 7 Fikiri sana kuhusu haya nisemayo, kwa maana Mwenyezi Mungu atakupa ufahamu katika mambo haya yote. \p \v 8 Mkumbuke Isa Al-Masihi aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yeye aliye wa uzao wa Daudi. Hii ndiyo Injili yangu, \v 9 ambayo kwayo ninateseka hata kufikia hatua ya kufungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu halifungwi. \v 10 Kwa hiyo ninavumilia mambo yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, kusudi wao nao wapate wokovu ulio katika Al-Masihi Isa, pamoja na utukufu wa milele. \p \v 11 Hili ni neno la kuaminiwa: \q1 Kama tumekufa pamoja naye, \q2 tutaishi pia pamoja naye. \q1 \v 12 Kama tukistahimili, \q2 pia tutatawala pamoja naye. \q1 Kama tukimkana, \q2 naye atatukana. \q1 \v 13 Tusipoaminika, \q2 yeye hudumu akiwa mwaminifu, \q2 kwa maana hawezi kujikana mwenyewe. \s1 Mtendakazi aliyekubaliwa na Mwenyezi Mungu \p \v 14 Endelea kuwakumbusha mambo haya, ukiwaonya mbele za Mungu waache kushindana kwa maneno ambayo hayana faida yoyote, bali huwaangamiza tu wale wanaoyasikia. \v 15 Jitahidi kujionesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli. \v 16 Jiepushe na maneno machafu yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kutomcha Mungu. \v 17 Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto, \v 18 ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kupita, nao hupindua imani ya baadhi ya watu. \v 19 Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, ukiwa na muhuri wenye maandishi haya: “Mwenyezi Mungu anawajua walio wake”; tena, “Kila alitajaye jina la Mwenyezi Mungu na auache uovu.” \p \v 20 Katika nyumba kubwa si kwamba kuna vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali pia vimo vyombo vya miti na vya udongo; vingine kwa matumizi maalum, na vingine kwa matumizi ya kawaida. \v 21 Basi ikiwa mtu amejitakasa na kujitenga na hayo niliyoyataja, atakuwa chombo maalum, kilichotengwa na ambacho kinamfaa mwenye nyumba, kimeandaliwa tayari kwa kila kazi njema. \p \v 22 Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana Isa kwa moyo safi. \v 23 Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa unajua hayo huzaa magomvi. \v 24 Tena haimpasi mtumishi wa Bwana Isa kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. \v 25 Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, \v 26 ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake. \c 3 \s1 Hatari za siku za mwisho \p \v 1 Lakini yakupasa ufahamu jambo hili: kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari. \v 2 Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu, \v 3 wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema, \v 4 wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wanaopenda anasa kuliko kumpenda Mungu: \v 5 wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje, lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu kama hao. \p \v 6 Miongoni mwao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu na kuwachukua mateka wanawake wajinga, waliolemewa na dhambi zao na kuyumbishwa na aina zote za tamaa mbaya. \v 7 Hawa hujifunza siku zote, lakini kamwe hawawezi kuufikia ujuzi wa kweli. \v 8 Kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo watu hawa hupingana na kweli. Hawa ni watu wenye akili zilizopotoka, ambao wamekataliwa kwa mambo ya imani. \v 9 Lakini hawataendelea sana, kwa sababu upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile upumbavu wa hao watu wawili ulivyokuwa dhahiri. \s1 Paulo amwagiza Timotheo \p \v 10 Lakini wewe umeyajua mafundisho yangu, mwenendo, makusudi, imani, uvumilivu, upendo, ustahimilivu, \v 11 mateso na taabu, yaani mambo yote yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Listra, mateso yote niliyostahimili, lakini Bwana Isa aliniokoa katika hayo yote. \v 12 Naam, yeyote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Al-Masihi Isa atateswa. \v 13 Lakini watu waovu na wadanganyaji watazidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. \v 14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, \v 15 na jinsi tangu utoto umeyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kupitia kwa imani katika Al-Masihi Isa. \v 16 Maandiko yote yamevuviwa na Mungu, na yafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, \v 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema. \c 4 \s1 Maagizo ya mwisho \p \v 1 Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Al-Masihi Isa, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba: \v 2 Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri. \v 3 Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima. Badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu watakaowaambia yale masikio yao yanatamani kusikia. \v 4 Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo. \v 5 Bali wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako. \p \v 6 Kwa maana mimi sasa ni tayari kumiminwa kama sadaka ya kinywaji, nayo saa yangu ya kuondoka imetimia. \v 7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda. \v 8 Sasa nimewekewa taji la haki ambalo Bwana, Mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile: wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake. \s1 Maelekezo ya binafsi \p \v 9 Jitahidi kuja kwangu upesi \v 10 kwa sababu Dema, kwa kuupenda ulimwengu, ameniacha na ameenda Thesalonike. Kreske ameenda Galatia, na Tito ameenda Dalmatia. \v 11 Ni Luka pekee aliye hapa nami. Mtafute Marko uje naye, kwa sababu ananifaa sana katika huduma yangu. \v 12 Nimemtuma Tikiko huko Efeso. \v 13 Utakapokuja, niletee lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, na vile vitabu vyangu, hasa vile vya ngozi. \p \v 14 Iskanda yule mfua chuma alinitendea ubaya mkubwa. Bwana Isa atamlipa kwa ajili ya yale aliyotenda. \v 15 Wewe pia ujihadhari naye kwa sababu aliyapinga maneno yetu vikali. \p \v 16 Katika utetezi wangu wa mara ya kwanza, hakuna hata mmoja aliyeniunga mkono, bali kila mmoja aliniacha. Naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. \v 17 Lakini Bwana Isa alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kupitia kwangu lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka kinywa cha simba. \v 18 Bwana Isa ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe milele na milele. Amen. \b \s1 Salamu za mwisho \p \v 19 Wasalimu Prisila\f + \fr 4:19 \fr*\ft kwa Kiyunani ni \ft*\fqa Priska\fqa*\f* na Akila, na wote wa nyumbani mwa Onesiforo. \b \p \v 20 Erasto alibaki Korintho, nami nikamwacha Trofimo huko Mileto akiwa mgonjwa. \v 21 Jitahidi ufike huku kabla ya majira ya baridi. \b \p Eubulo anakusalimu, vivyo hivyo Pude, Lino, Klaudia na ndugu wote. \b \p \v 22 Bwana Isa awe pamoja na roho yako. Neema iwe pamoja nanyi.