\id 1SA - Biblica® Open Kiswahili Contemporary Scriptures (Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu) \ide UTF-8 \h 1 Samweli \toc1 1 Samweli \toc2 1 Samweli \toc3 1Sam \mt1 1 Samweli \c 1 \s1 Kuzaliwa kwa Samweli \p \v 1 Kulikuwa na mtu mmoja kutoka Rama, Msufi kutoka nchi ya vilima ya Efraimu, aliyeitwa Elkana mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu mwana wa Tohu, mwana wa Sufu Mwefraimu. \v 2 Alikuwa na wake wawili; mmoja aliitwa Hana na mwingine Penina. Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na mtoto. \p \v 3 Kila mwaka mtu huyu alikwea kutoka mji wake ili kuabudu na kutoa dhabihu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni huko Shilo, ambapo Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwa makuhani wa Mwenyezi Mungu. \v 4 Kila mara ilipofika siku ya Elkana kutoa dhabihu, aliwapa mafungu Penina mkewe na wanawe wote wa kiume na wa kike. \v 5 Lakini alimpa Hana fungu maradufu kwa sababu alimpenda, ingawa Mwenyezi Mungu alikuwa amemfunga tumbo. \v 6 Kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amemfunga tumbo, mke mwenzake alikuwa anamchokoza ili kumuudhi. \v 7 Hili liliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipoenda katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, mke mwenzake alikuwa akimkasirisha hadi analia na kushindwa kula. \v 8 Elkana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?” \p \v 9 Siku moja walipokuwa wamemaliza kula na kunywa huko Shilo, Hana alisimama. Wakati huo kuhani Eli alikuwa ameketi kwenye kiti pembeni mwa mwimo wa mlango wa Hekalu la Mwenyezi Mungu. \v 10 Kwa uchungu wake mwingi Hana alimwomba Mwenyezi Mungu, akilia kwa uchungu. \v 11 Naye akaweka nadhiri, akisema, “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, laiti ungeangalia huzuni kuu ya mtumishi wako na kunikumbuka mimi, wala usimsahau mtumishi wako nawe ukampa mwana, basi huyo mwana nitamtoa kwa Mwenyezi Mungu kwa siku zote za maisha yake, wala wembe hautapita kichwani mwake.” \p \v 12 Alipokuwa anaendelea kumwomba Mwenyezi Mungu, Eli alichunguza kinywa chake. \v 13 Hana alikuwa akiomba moyoni mwake, midomo yake ikiwa inachezacheza lakini sauti haikusikika. Eli akafikiri alikuwa amelewa \v 14 naye akamwambia, “Utaendelea kulewa hadi lini? Achilia mbali mvinyo wako.” \p \v 15 Hana akajibu, “Si hivyo bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye huzuni kubwa. Mimi sijanywa mvinyo wala kileo, nilikuwa ninaumimina moyo wangu kwa Mwenyezi Mungu. \v 16 Usimdhanie mtumishi wako kuwa mwanamke mwovu; nimekuwa nikiomba hapa kutokana na uchungu mkuu na huzuni.” \p \v 17 Eli akamjibu, “Nenda kwa amani, naye Mungu wa Israeli na akujalie kile ulichomwomba.” \p \v 18 Hana akasema, “Mtumishi wako na apate kibali machoni pako.” Kisha akaondoka zake na kula chakula, wala uso wake haukuwa na huzuni tena. \p \v 19 Kesho yake asubuhi na mapema waliamka wakaabudu mbele za Mwenyezi Mungu na kisha wakarudi nyumbani mwao huko Rama. Elkana akakutana kimwili na mkewe Hana, naye Mwenyezi Mungu akamkumbuka. \v 20 Hivyo wakati ulipotimia, Hana akapata mimba na akamzaa mwana. Hana akamwita jina Samweli, akisema, “Kwa kuwa nilimwomba kwa Mwenyezi Mungu.” \s1 Hana amweka Samweli wakfu \p \v 21 Huyo mtu Elkana alipopanda pamoja na jamaa yake yote kutoa dhabihu ya mwaka kwa Mwenyezi Mungu na kutimiza nadhiri yake, \v 22 Hana hakuenda. Alimwambia mume wake, “Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, nitamchukua na kumpeleka mbele za Mwenyezi Mungu, naye ataishi huko daima.” \p \v 23 Elkana mumewe akamwambia, “Fanya lile unaloona ni bora zaidi kwako. Ukae hapa hadi utakapomwachisha kunyonya, Mwenyezi Mungu na akujalie kutimiza nadhiri yako.” Hivyo huyo mwanamke akakaa nyumbani na kumnyonyesha mwanawe hadi alipomwachisha kunyonya. \p \v 24 Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, Hana akamchukua huyo mtoto, akiwa mdogo hivyo hivyo, pamoja na fahali wa miaka mitatu, efa ya unga\f + \fr 1:24 \fr*\ft Efa moja ya unga ni sawa na kilo 22.\ft*\f* na kiriba cha divai, naye akamleta mtoto kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Shilo. \v 25 Walipokwisha kumchinja yule fahali, wakamleta mtoto kwa Eli, \v 26 naye Hana akamwambia Eli, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu, mimi ndiye yule mama ambaye alisimama hapa karibu nawe akiomba kwa Mwenyezi Mungu. \v 27 Niliomba mtoto huyu, naye Mwenyezi Mungu amenijalia kile nilichomwomba. \v 28 Hivyo sasa ninamtoa kwa Mwenyezi Mungu. Kwa maana maisha yake yote atakuwa ametolewa kwa Mwenyezi Mungu.” Naye akamwabudu Mwenyezi Mungu huko. \c 2 \s1 Maombi ya Hana \p \v 1 Kisha Hana akaomba na kusema: \q1 “Moyo wangu wamshangilia Mwenyezi Mungu, \q2 katika Mwenyezi Mungu pembe\f + \fr 2:1 \fr*\ft pembe inawakilisha nguvu\ft*\f* yangu imeinuliwa juu. \q1 Kinywa changu chajisifu juu ya adui zangu, \q2 kwa kuwa naufurahia wokovu wako. \b \q1 \v 2 “Hakuna yeyote aliye mtakatifu kama Mwenyezi Mungu, \q2 hakuna mwingine zaidi yako; \q2 hakuna Mwamba kama Mungu wetu. \b \q1 \v 3 “Msiendelee kusema kwa kiburi hivyo \q2 wala msiache vinywa vyenu kunena kwa kiburi, \q1 kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu ajuaye, \q2 na yeye hupima matendo. \b \q1 \v 4 “Pinde za mashujaa zimevunjika, \q2 lakini wale wanaojikwaa wamevikwa nguvu. \q1 \v 5 Wale waliokuwa na chakula tele wamejikodisha wenyewe \q2 ili kupata chakula, \q1 lakini wale waliokuwa na njaa \q2 hawana njaa tena. \q1 Mwanamke yule aliyekuwa tasa \q2 amezaa watoto saba, \q1 lakini yule aliyekuwa na wana wengi \q2 amedhoofika. \b \q1 \v 6 “Mwenyezi Mungu huua na huhuisha; \q2 yeye hushusha hadi kaburini\f + \fr 2:6 \fr*\ft Kaburini maana yake ni \ft*\fqa Kuzimu\fqa*\ft ; kwa Kiebrania ni \ft*\fqa Sheol.\fqa*\f* na hufufua. \q1 \v 7 Mwenyezi Mungu humfanya mtu maskini naye hutajirisha, \q2 hushusha na hukweza. \q1 \v 8 Humwinua maskini kutoka mavumbini \q2 na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu; \q1 huwaketisha pamoja na wakuu, \q2 na kuwafanya warithi kiti cha utawala cha heshima. \b \q1 “Kwa kuwa misingi ya dunia ni ya Mwenyezi Mungu; \q2 juu yake ameuweka ulimwengu. \q1 \v 9 Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake, \q2 lakini waovu watanyamazishwa kwenye giza. \b \q1 “Si kwa nguvu mtu hushinda; \q2 \v 10 wale wampingao Mwenyezi Mungu \q2 wataharibiwa kabisa. \q1 Atapiga radi dhidi yao kutoka mbinguni; \q2 Mwenyezi Mungu ataihukumu miisho ya dunia. \b \q1 “Atampa nguvu mfalme wake, \q2 na kuitukuza pembe \q2 ya mpakwa mafuta wake.” \p \v 11 Kisha Elkana akaenda nyumbani Rama, lakini mtoto akahudumu mbele za Mwenyezi Mungu chini ya kuhani Eli. \s1 Wana Waovu wa Eli \p \v 12 Wana wa Eli walikuwa watu waovu kabisa, hawakumheshimu Mwenyezi Mungu. \v 13 Basi ilikuwa desturi ya makuhani pamoja na watu kwamba kila mara yeyote anapotoa dhabihu na huku nyama ikiwa inachemshwa, mtumishi wa kuhani angekuja na uma wenye meno matatu mkononi mwake. \v 14 Angeutumbukiza huo uma kwenye sufuria au birika au sufuria kubwa au chungu, naye kuhani angejichukulia chochote uma ungekileta. Hivi ndivyo walivyowatendea Waisraeli wote waliokuja Shilo. \v 15 Lakini hata kabla mafuta ya mnyama hayajachomwa, mtumishi wa kuhani angekuja na kusema kwa mtu aliyekuwa akitoa dhabihu, “Mpe kuhani nyama akaoke, kwani hatapokea nyama iliyochemshwa kutoka kwako, ila iliyo mbichi tu.” \p \v 16 Mtu yule akimwambia, “Mafuta ya mnyama na yachomwe kwanza, ndipo uchukue chochote unachotaka,” mtumishi angejibu, “Hapana, nipe sasa; kama hunipi, nitaichukua kwa nguvu.” \p \v 17 Hii dhambi ya hawa vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa waliitendea dhabihu ya Mwenyezi Mungu kwa dharau. \p \v 18 Lakini Samweli alikuwa akihudumu mbele za Mwenyezi Mungu, kijana akivaa kizibau cha kitani. \v 19 Kila mwaka mama yake alimshonea joho dogo na kumpelekea alipokwea pamoja na mumewe kutoa dhabihu ya mwaka. \v 20 Eli alikuwa akiwabariki Elkana na mkewe, akisema, “Mwenyezi Mungu na akupe watoto kwa mwanamke huyu ili kuchukua nafasi ya yule aliyekuwa amemwomba na akamtoa kwa Mwenyezi Mungu.” Kisha wakawa wanaenda nyumbani. \v 21 Mwenyezi Mungu akawa mwenye neema kwa Hana, naye akapata mimba akazaa wana wa kiume watatu na binti wawili. Wakati huo, kijana Samweli akaendelea kukua mbele za Mwenyezi Mungu. \p \v 22 Basi Eli, aliyekuwa mzee sana, alisikia kuhusu kila kitu ambacho wanawe walikuwa wakiwafanyia Israeli wote na jinsi walivyokutana kimwili na wanawake waliohudumu kwenye ingilio la Hema la Kukutania. \v 23 Hivyo akawaambia, “Kwa nini mmefanya mambo kama haya? Nimesikia kutoka kwa watu wote kuhusu haya matendo yenu maovu. \v 24 Sivyo, wanangu, hii si habari nzuri ninayosikia ikienea miongoni mwa watu wa Mwenyezi Mungu. \v 25 Mtu akifanya dhambi dhidi ya mtu mwenzake, mtu mwingine aweza kumwombea kwa Mungu, lakini kama mtu akimfanyia Mungu dhambi, ni nani atakayemwombea?” Hata hivyo wanawe hawakusikia maonyo ya baba yao, kwa sababu Mwenyezi Mungu alitaka kuwaua. \p \v 26 Naye kijana Samweli akaendelea kukua katika kimo, akimpendeza Mwenyezi Mungu na wanadamu. \s1 Unabii dhidi ya nyumba ya Eli \p \v 27 Basi mtu wa Mungu akaja kwa Eli na kumwambia, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Je, sikujifunua waziwazi kwa nyumba ya baba yako wakati walikuwa huko Misri chini ya Farao? \v 28 Nilimchagua baba yako kati ya makabila yote ya Israeli kuwa kuhani wangu, kukwea kwenye madhabahu yangu, kufukiza uvumba na kuvaa kizibau mbele yangu. Pia niliwapa nyumba ya baba yako sadaka zote zilizotolewa kwa moto na Waisraeli. \v 29 Kwa nini unadharau dhabihu zangu na sadaka nilizoziamuru kwa ajili ya makao yangu? Kwa nini unawaheshimu wanao kuliko mimi kwa kujinenepesha wenyewe kwa kula sehemu zilizo bora za kila sadaka zinazotolewa na watu wangu wa Israeli?’ \p \v 30 “Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asema: ‘Niliahidi kuwa nyumba yako na nyumba ya baba yako wangehudumu mbele zangu milele.’ Lakini sasa Mwenyezi Mungu anasema: ‘Jambo hili na liwe mbali nami! Wale wanaoniheshimu nitawaheshimu, wale wanaonidharau mimi watadharauliwa. \v 31 Wakati unakuja nitakapozipunguza nguvu zenu na nguvu ya nyumba ya baba yenu, ili pasiwepo mtu katika jamaa yenu atakayeishi kuuona uzee, \v 32 nanyi mtaona huzuni katika makao yangu. Ingawa Israeli watatendewa mema, katika jamaa yenu kamwe hapatakuwa na mtu atakayeishi hadi kuwa mzee. \v 33 Kila mmoja wenu ambaye sitamkatilia mbali kutoka madhabahuni pangu atabakizwa tu kupofusha macho yenu kwa machozi na kuihuzunisha mioyo yenu, nao wazao wenu wote watakufa watakapokuwa wamefikia umri wa kustawi. \p \v 34 “ ‘Kile kitakachotokea kwa wanao wawili, Hofni na Finehasi, kitakuwa ishara kwako. Wote wawili watakufa katika siku moja. \v 35 Mimi mwenyewe nitajiinulia kuhani mwaminifu, ambaye atafanya sawasawa na kile kilichoko moyoni mwangu na akilini mwangu. Nitaiimarisha nyumba yake ya ukuhani, naye atahudumu mbele ya mpakwa mafuta wangu daima. \v 36 Kisha kila mmoja aliyeachwa katika jamaa yenu atakuja na kusujudu mbele yake kwa ajili ya kipande cha fedha na ganda la mkate, akisema, “Niteue katika baadhi ya ofisi ya ukuhani ili niweze kupata chakula.” ’ ” \c 3 \s1 Mwenyezi Mungu amwita Samweli \p \v 1 Kijana Samweli alihudumu mbele za Mwenyezi Mungu chini ya Eli. Katika siku zile neno la Mungu lilikuwa adimu, hapakuwa na maono mengi. \p \v 2 Usiku mmoja Eli, ambaye macho yake yalikuwa yamefifia sana kiasi kwamba aliona kwa shida sana, alikuwa amelala mahali pake pa kawaida. \v 3 Taa ya Mungu bado ilikuwa haijazimika, na Samweli alikuwa amelala hekaluni\f + \fr 3:3 \fr*\ft Hekaluni maana yake ndani ya Maskani ya Mwenyezi Mungu.\ft*\f* mwa Mwenyezi Mungu, ambapo Sanduku la Mungu lilikuwa. \v 4 Kisha Mwenyezi Mungu akamwita Samweli. \p Samweli akajibu, “Mimi hapa.” \v 5 Naye akakimbia kwa Eli na kumwambia, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.” \p Lakini Eli akasema, “Sikukuita; rudi ukalale.” Hivyo akaenda kulala. \p \v 6 Mwenyezi Mungu akaita tena, “Samweli!” Naye Samweli akaamka, kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.” \p Eli akasema, “Mwanangu, sikukuita, rudi ukalale.” \p \v 7 Wakati huu Samweli alikuwa bado hajamjua Mwenyezi Mungu. Neno la Mwenyezi Mungu lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. \p \v 8 Mwenyezi Mungu akamwita Samweli mara ya tatu, naye Samweli akaamka kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.” \p Ndipo Eli akatambua kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa akimwita kijana. \v 9 Hivyo Eli akamwambia Samweli, “Nenda ukalale; akikuita, sema, ‘Nena Mwenyezi Mungu, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.’ ” Hivyo Samweli akaenda na kulala mahali pake. \p \v 10 Mwenyezi Mungu akaja, akasimama pale, akiita kama hapo awali, “Samweli! Samweli!” \p Kisha Samweli akasema, “Nena Mwenyezi Mungu, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.” \p \v 11 Naye Mwenyezi Mungu akamwambia Samweli: “Tazama, nipo karibu kufanya kitu katika Israeli ambacho kitafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia yawashe. \v 12 Wakati huo nitatimiza dhidi ya Eli kila kitu nilichonena dhidi ya jamaa yake, kuanzia mwanzo hadi mwisho. \v 13 Kwa kuwa nilimwambia kwamba ningehukumu jamaa yake milele kwa sababu ya dhambi aliyoijua, wanawe kumkufuru Mungu, naye akashindwa kuwazuia. \v 14 Kwa hiyo, nikaapa kuhusu nyumba ya Eli, ‘Hatia ya nyumba ya Eli kamwe haitaweza kufidiwa kwa dhabihu au sadaka.’ ” \p \v 15 Samweli akalala hadi asubuhi, kisha akafungua milango ya nyumba ya Mwenyezi Mungu. Aliogopa kumwambia Eli yale maono, \v 16 lakini Eli akamwita na kumwambia, “Samweli mwanangu.” \p Samweli akamjibu, “Mimi hapa.” \p \v 17 Eli akamuuliza, “Ni nini alichokuambia? Usinifiche. Mwenyezi Mungu na akuadhibu vikali zaidi kama utanificha chochote alichokuambia.” \v 18 Kwa hiyo Samweli akamwambia kila kitu bila kumficha chochote. Ndipo Eli akasema, “Yeye ni Mwenyezi Mungu; na afanye lile lililo jema machoni pake!” \p \v 19 Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Samweli alipokuwa akikua, na hakuacha neno lolote la Samweli lianguke chini. \v 20 Nao Israeli wote kuanzia Dani hadi Beer-Sheba wakatambua kuwa Samweli amethibitishwa kuwa nabii wa Mwenyezi Mungu. \v 21 Mwenyezi Mungu akaendelea kutokea huko Shilo, na huko alijidhihirisha kwa Samweli kupitia neno lake. \c 4 \p \v 1 Nalo neno la Samweli likaja kwa Israeli yote. \s1 Wafilisti wateka Sanduku la Mungu \p Basi Waisraeli walitoka kwenda kupigana dhidi ya Wafilisti. Waisraeli wakapiga kambi huko Ebenezeri, nao Wafilisti wakapiga kambi huko Afeki. \v 2 Wafilisti wakapanga safu za majeshi yao kupambana na Israeli, wakati vita vilipoenea, Israeli wakashindwa na Wafilisti, ambao waliwaua askari wa Israeli wapatao elfu nne kwenye uwanja wa vita. \v 3 Askari waliporudi kambini, wazee wa Israeli wakawauliza, “Kwa nini Mwenyezi Mungu ameruhusu leo tushindwe mbele ya Wafilisti? Tuleteni Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu kutoka Shilo, ili lipate kwenda pamoja nasi, na kutuokoa kutoka mikono ya adui zetu.” \p \v 4 Hivyo wakawatuma watu huko Shilo, nao wakalichukua Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, aliyekaa kwenye kiti chake cha enzi kati ya makerubi. Nao Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, walikuwa huko na Sanduku la Agano la Mungu. \p \v 5 Wakati Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu lilikuja kambini, Waisraeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu hata ardhi ikatikisika. \v 6 Wafilisti waliposikia makelele, wakauliza, “Kwa nini kuna makelele haya yote katika kambi ya Waebrania?” \p Walipofahamu kuwa Sanduku la Mwenyezi Mungu limekuja kambini, \v 7 Wafilisti wakaogopa, wakasema, “Mungu amekuja kambini, ole wetu. Halijatokea jambo kama hili tangu hapo awali. \v 8 Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa kutoka mikononi mwa miungu hii yenye nguvu? Ni miungu ile iliyowapiga Wamisri kwa mapigo ya aina zote huko jangwani. \v 9 Tuweni hodari, enyi Wafilisti! Tuweni wanaume, la sivyo mtakuwa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa kwenu. Kuweni wanaume, mpigane!” \p \v 10 Basi Wafilisti wakapigana, nao Waisraeli wakashindwa na kila mtu akakimbilia kwenye hema lake. Mauaji yalikuwa makubwa sana, Israeli wakapoteza askari elfu thelathini walioenda kwa miguu. \v 11 Sanduku la Mungu likatekwa, na hao wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa. \s1 Kifo cha Eli \p \v 12 Siku ile ile mtu mmoja wa kabila la Benyamini akakimbia kutoka uwanja wa vita na kwenda Shilo, nguo zake zikiwa zimeraruka na akiwa na mavumbi kichwani mwake. \v 13 Alipofika, Eli alikuwa ameketi kwenye kiti chake kando ya barabara akiangalia, kwa sababu moyo wake ulikuwa na hofu kwa ajili ya Sanduku la Mungu. Mtu yule alipoingia mjini na kueleza kilichokuwa kimetokea, mji wote ukalia. \p \v 14 Eli akasikia kelele za kilio, naye akauliza, “Ni nini maana ya makelele haya?” \p Yule mtu akafanya haraka kwenda kwa Eli, \v 15 wakati huu Eli alikuwa na umri wa miaka tisini na nane, nayo macho yake yalikuwa yamepofuka hadi hakuweza kuona. \v 16 Akamwambia Eli, “Mimi nimetoka vitani sasa hivi, nimekimbia kutoka huko siku ya leo.” \p Eli akamuuliza, “Je, mwanangu, ni nini kimetokea huko?” \p \v 17 Yule mtu aliyeleta habari akajibu, “Waisraeli wamekimbia mbele ya Wafilisti, na wanajeshi wengi sana wameuawa. Pia wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa, na Sanduku la Mungu limetekwa.” \p \v 18 Mara alipotaja Sanduku la Mungu, Eli alianguka kwa nyuma kutoka kiti chake kando ya lango. Shingo yake ikavunjika naye akafa, kwa kuwa alikuwa mzee tena mzito. Alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka arobaini. \p \v 19 Mkwewe, mke wa Finehasi, alikuwa mjamzito na alikaribia wakati wa kujifungua. Aliposikia habari kwamba Sanduku la Mungu limetekwa na ya kuwa baba mkwe wake na mumewe wamekufa, akapata uchungu naye akajifungua lakini akazidiwa na uchungu. \v 20 Alipokuwa akifa, wanawake waliokuwa wanamhudumia wakamwambia, “Usiogope, umemzaa mwana wa kiume.” Lakini hakujibu wala kuweka maanani. \p \v 21 Alimwita yule mtoto Ikabodi\f + \fr 4:21 \fr*\ft maana yake \ft*\fqa Utukufu umeondoka\fqa*\f*, akisema, “Utukufu umeondoka katika Israeli,” kwa sababu ya kutekwa kwa Sanduku la Mungu na vifo vya baba mkwe na mumewe. \v 22 Akasema, “Utukufu umeondoka katika Israeli, kwa kuwa Sanduku la Mungu limetekwa.” \c 5 \s1 Sanduku la Agano huko Ashdodi na Ekroni \p \v 1 Baada ya Wafilisti kuteka Sanduku la Mungu, walilichukua kutoka Ebenezeri hadi Ashdodi. \v 2 Kisha wakaliingiza lile Sanduku ndani ya hekalu la Dagoni na kuliweka kando ya huyo Dagoni. \v 3 Watu wa Ashdodi walipoamka asubuhi na mapema kesho yake, kumbe, wakamkuta Dagoni ameanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu! Wakamwinua Dagoni na kumrudisha mahali pake. \v 4 Lakini asubuhi iliyofuata, walipoamka kumbe, walimkuta Dagoni ameanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu! Kichwa chake na mikono vilikuwa vimevunjwa, navyo vimelala kizingitini; ni kiwiliwili chake tu kilichokuwa kimebaki. \v 5 Ndiyo sababu hadi leo makuhani wa Dagoni na wengine wanaoingia katika hekalu la Dagoni huko Ashdodi hawakanyagi kizingiti. \p \v 6 Mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi na vijiji jirani, akaleta uharibifu juu yao na kuwatesa kwa majipu. \v 7 Watu wa Ashdodi walipoona kile kilichokuwa kikitokea, wakasema, “Sanduku la Mungu wa Israeli kamwe lisikae hapa pamoja na sisi, kwa sababu mkono wake ni mzito juu yetu na juu ya Dagoni mungu wetu.” \v 8 Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kuwauliza, “Tutafanya nini na hili Sanduku la Mungu wa Israeli?” \p Wakajibu, “Sanduku la Mungu wa Israeli na liende Gathi.” Basi wakalihamisha Sanduku la Mungu wa Israeli. \p \v 9 Lakini baada ya kulihamisha, mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa dhidi ya huo mji wa Gathi, akiuweka katika fadhaa kuu. Mungu akawatesa watu wa huo mji, vijana kwa wazee, kwa kuwaletea majipu. \v 10 Basi wakapeleka Sanduku la Mungu Ekroni. \p Sanduku la Mungu lilipokuwa linaingia Ekroni, watu wa Ekroni walilia wakisema, “Wamelileta Sanduku la Mungu wa Israeli kwetu ili kutuua sisi na watu wetu.” \v 11 Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kusema, “Liondoeni Sanduku la Mungu wa Israeli na lirudishwe mahali pake, la sivyo litatuua sisi na watu wetu.” Kwa kuwa kifo kilikuwa kimeujaza mji hofu; kwani mkono wa Mungu ulikuwa mzito sana juu yake. \v 12 Wale ambao hawakufa walipatwa na majipu, na kilio cha mji kilifika hadi mbinguni. \c 6 \s1 Sanduku la Mungu larudishwa Israeli \p \v 1 Sanduku la Mwenyezi Mungu lilipokuwa limekaa katika nchi ya Wafilisti kwa miezi saba, \v 2 Wafilisti waliwaita makuhani wa Dagoni na waaguzi, na kuwaambia, “Tutafanya nini na hili Sanduku la Mwenyezi Mungu? Tuambieni jinsi tutakavyolirudisha mahali pake.” \p \v 3 Wakajibu, “Kama mtalirudisha Sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe mikono mitupu bali kwa vyovyote mpelekeeni sadaka ya hatia. Kisha mtaponywa, nanyi mtafahamu kwa nini mkono wake haujaondolewa kwenu.” \p \v 4 Wafilisti wakawauliza, “Ni sadaka gani ya hatia tutakayompelekea?” \p Wakajibu, “Majipu matano ya dhahabu na panya wa dhahabu watano, kulingana na idadi ya watawala wa Wafilisti, kwa sababu tauni hiyo hiyo imewadhuru ninyi na watawala wenu. \v 5 Tengenezeni mifano ya majipu na ya panya wale wanaoharibu nchi yenu, nanyi mtukuzeni Mungu wa Israeli. Labda ataondoa mkono wake kutoka kwenu na kwa miungu yenu na nchi yenu. \v 6 Kwa nini ninyi mnafanya mioyo yenu migumu kama Wamisri na Farao walivyofanya? Je, alipowatendea kwa ukali, hawakuwaachia Waisraeli wakaenda zao? \p \v 7 “Sasa basi, wekeni gari jipya la kukokotwa pamoja na ng’ombe wawili ambao wamezaa lakini ambao kamwe hawajafungwa nira. Fungieni hao ng’ombe hilo gari, lakini ondoeni ndama wao na mwaweke zizini. \v 8 Chukueni hilo Sanduku la Mwenyezi Mungu na mliweke juu ya gari la kukokotwa, na ndani ya kasha kando yake wekeni hivyo vitu vya dhahabu mnavyompelekea Mwenyezi Mungu kama sadaka ya hatia. Lipelekeni, \v 9 lakini liangalieni kwa makini. Iwapo litaenda katika nchi yake lenyewe, kuelekea Beth-Shemeshi, basi tutajua kwamba Mwenyezi Mungu ndiye alileta haya maafa makubwa juu yetu. Lakini kama halikwenda, basi tutajua kwamba haukuwa mkono wa Mwenyezi Mungu uliotupiga na kwamba iliyotokea kwetu ni ajali.” \p \v 10 Basi wakafanya hivyo. Wakachukua ng’ombe wawili wa aina hiyo, wakawafungia hilo gari la kukokotwa, nao ndama wao wakawekwa zizini. \v 11 Wakaliweka Sanduku la Mwenyezi Mungu juu ya hilo gari la kukokotwa pamoja na lile kasha lenye ile mifano ya panya wa dhahabu na ya majipu ya dhahabu. \v 12 Kisha hao ng’ombe wakaenda moja kwa moja kuelekea Beth-Shemeshi, wakishuka bila kugeuka kuume au kushoto, huku wakilia njia yote. Watawala wa Wafilisti waliwafuata hao ng’ombe hadi mpakani mwa Beth-Shemeshi. \p \v 13 Wakati huu watu wa Beth-Shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao huko bondeni, walipoinua macho yao na kuona lile Sanduku, wakafurahi kuliona. \v 14 Lile gari la kukokotwa lilikuja kwenye shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi, nalo likasimama kando ya mwamba mkubwa. Watu wakapasua mbao za lile gari la kukokotwa na kutoa dhabihu wale ng’ombe kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu. \v 15 Walawi walilishusha Sanduku la Mwenyezi Mungu, pamoja na lile kasha lililokuwa na vile vitu vya dhahabu na kuviweka juu ya ule mwamba mkubwa. Siku ile watu wa Beth-Shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu kwa Mwenyezi Mungu. \v 16 Wale watawala watano wa Wafilisti waliona haya yote, nao wakarudi Ekroni siku ile ile. \p \v 17 Haya ndio yale majipu ya dhahabu Wafilisti waliyotuma kama sadaka ya hatia kwa Mwenyezi Mungu: moja kwa ajili ya Ashdodi, moja kwa Gaza, moja kwa Ashkeloni, moja kwa Gathi, na moja kwa Ekroni. \v 18 Nayo hesabu ya wale panya wa dhahabu ilikuwa kulingana na idadi ya miji ya Wafilisti ya watawala watano wa Wafilisti: miji yao yenye ngome, pamoja na vijiji vya miji hiyo. Ule mwamba mkubwa, ambao juu yake waliliweka lile Sanduku la Mwenyezi Mungu, ni ushahidi hadi leo katika shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi. \p \v 19 Lakini Mungu aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-Shemeshi, akiwaua watu sabini miongoni mwao kwa sababu walichungulia ndani ya Sanduku la Mwenyezi Mungu. Watu wakaomboleza kwa sababu ya pigo zito kutoka kwa Mwenyezi Mungu, \v 20 nao watu wa Beth-Shemeshi wakauliza, “Ni nani awezaye kusimama mbele za Mwenyezi Mungu, huyu Mungu aliye mtakatifu? Sanduku litapanda kwenda kwa nani kutoka hapa?” \p \v 21 Kisha wakatuma wajumbe kwa watu wa Kiriath-Yearimu, wakisema, “Wafilisti wamerudisha Sanduku la Mwenyezi Mungu. Shukeni na mlipandishe huko kwenu.” \c 7 \p \v 1 Kisha wanaume wa Kiriath-Yearimu wakaja na kulichukua Sanduku la Mwenyezi Mungu. Wakalipeleka katika nyumba ya Abinadabu kilimani, na kumweka Eleazari mwanawe wakfu kulichunga Sanduku la Mwenyezi Mungu. \p \v 2 Sanduku la Mwenyezi Mungu lilibakia huko Kiriath-Yearimu kwa muda mrefu, jumla ya miaka ishirini. \s1 Samweli awatiisha Wafilisti huko Mispa \p Nao watu wote wa Israeli wakamrudia Mwenyezi Mungu. \v 3 Naye Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, “Ikiwa mtamrudia Mwenyezi Mungu kwa mioyo yenu yote, basi iacheni miungu migeni na Maashtorethi, na kujitoa wenyewe kwa Mwenyezi Mungu na kumtumikia yeye peke yake, naye atawaokoa ninyi kutoka kwa mkono wa Wafilisti.” \v 4 Hivyo Waisraeli wakaweka mbali Mabaali yao na Maashtorethi yao, nao wakamtumikia Mwenyezi Mungu peke yake. \p \v 5 Kisha Samweli akasema, “Wakusanyeni Israeli wote huko Mispa, nami nitawaombea kwa Mwenyezi Mungu.” \v 6 Walipokwisha kukutanika huko Mispa, walichota maji na kuyamimina mbele za Mwenyezi Mungu. Siku hiyo walifunga na wakaungama, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu.” Naye Samweli alikuwa kiongozi\f + \fr 7:6 \fr*\ft yaani \ft*\fqa mwamuzi\fqa*\f* wa Israeli huko Mispa. \p \v 7 Wafilisti waliposikia kwamba Israeli wamekusanyika huko Mispa, watawala wa Wafilisti wakapanda ili kuwashambulia. Waisraeli waliposikia habari hiyo, waliogopa kwa sababu ya Wafilisti. \v 8 Wakamwambia Samweli, “Usiache kumlilia Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa ajili yetu, ili apate kutuokoa na mikono ya Wafilisti.” \v 9 Kisha Samweli akamchukua mwana-kondoo anyonyaye na kumtoa mzima kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu. Akamlilia Mwenyezi Mungu kwa niaba ya Israeli, naye Mwenyezi Mungu akamjibu. \p \v 10 Samweli alipokuwa anatoa hiyo dhabihu ya kuteketezwa, Wafilisti wakasogea karibu ili kupigana vita na Israeli. Lakini siku ile Mwenyezi Mungu alinguruma kwa ngurumo kubwa dhidi ya Wafilisti na kuwafanya wafadhaike na kutetemeka hivi kwamba walikimbizwa mbele ya Waisraeli. \v 11 Wanaume wa Israeli wakatoka mbio huko Mispa na kuwafuatia Wafilisti, wakiwachinja njiani hadi mahali chini ya Beth-Kari. \p \v 12 Ndipo Samweli akachukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni. Akaliita Ebenezeri\f + \fr 7:12 \fr*\ft maana yake \ft*\fqa Jiwe la usaidizi\fqa*\f*, akisema, “Hadi sasa Mwenyezi Mungu ametusaidia.” \v 13 Basi Wafilisti wakashindwa na hawakuvamia nchi ya Israeli tena. \p Katika maisha yote ya Samweli, mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa dhidi ya Wafilisti. \v 14 Miji kuanzia Ekroni hadi Gathi, ambayo Wafilisti walikuwa wameiteka kutoka Israeli, ilirudishwa kwake, naye Israeli akazikomboa nchi jirani mikononi mwa Wafilisti. Kukawa na amani kati ya Israeli na Waamori. \p \v 15 Samweli akaendelea kuwa mwamuzi wa Israeli siku zote za maisha yake. \v 16 Mwaka hadi mwaka aliendelea kuzunguka kutoka Betheli hadi Gilgali na Mispa, akiamua Israeli katika sehemu hizo zote. \v 17 Lakini kila mara alirudi Rama, kulikokuwa nyumbani mwake, huko pia aliamua Israeli. Naye huko alimjengea Mwenyezi Mungu madhabahu. \c 8 \s1 Israeli waomba mfalme \p \v 1 Samweli alipokuwa mzee, akaweka wanawe kuwa waamuzi wa Israeli. \v 2 Mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli, na wa pili aliitwa Abiya, nao wakatumika huko Beer-Sheba. \v 3 Lakini wanawe hawakuenenda katika njia zake. Waliziacha wakageukia faida za udanganyifu nao wakapokea rushwa na kupotosha haki. \p \v 4 Basi wazee wote wa Israeli wakakusanyika pamoja na kumjia Samweli huko Rama. \v 5 Wakamwambia, “Wewe umekuwa mzee, nao wanao hawaenendi katika njia zako, sasa tuteulie mfalme wa kutuongoza, kama ilivyo kwa mataifa mengine yote.” \p \v 6 Lakini wao waliposema, “Tupe mfalme wa kutuongoza,” hili lilimchukiza Samweli, hivyo akamwomba Mwenyezi Mungu. \v 7 Naye Mwenyezi Mungu akamwambia: “Sikiliza yale yote watu wanakuambia. Si wewe ambaye wamekukataa, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme wao. \v 8 Kama vile walivyofanya tangu siku nilipowapandisha kutoka Misri hadi siku hii ya leo; wakiniacha mimi na kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokufanyia wewe. \v 9 Sasa wasikilize, lakini waonye sana, na uwafahamishe yale watakayotendewa na mfalme atakayewatawala.” \p \v 10 Samweli akawaambia wale watu waliokuwa wakiomba wapewe mfalme maneno yote ya Mwenyezi Mungu. \v 11 Akasema, “Hivi ndivyo atakavyowatendea mfalme atakayewatawala. Atawachukua wana wenu na kuwafanya watumike kwa magari yake ya vita na farasi, nao watakimbia mbele ya magari yake. \v 12 Baadhi yao atawaweka kuwa majemadari wa jeshi wa maelfu na majemadari wa jeshi wa hamsini, wengine kulima mashamba yake na kuvuna mavuno yake, pia na wengine kutengeneza silaha za vita na vifaa kwa ajili ya magari yake ya vita. \v 13 Atawachukua binti zenu kuwa watengeneza manukato, wapishi na waokaji. \v 14 Atayachukua mashamba yenu yaliyo mazuri, mashamba ya mizabibu na mashamba yenu ya mizeituni na kuwapa watumishi wake. \v 15 Ataichukua sehemu ya kumi ya nafaka yenu na ya zabibu zenu na kuwapa maafisa wake na watumishi wake. \v 16 Atawachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike, na ng’ombe wenu walio wazuri sana na punda kwa matumizi yake mwenyewe. \v 17 Atachukua sehemu ya kumi ya makundi yenu ya kondoo na mbuzi, na ninyi wenyewe mtakuwa watumwa wake. \v 18 Siku ile itakapowadia, mtalia kwa kutaka msaada kutokana na mfalme mliyemchagua, naye Mwenyezi Mungu hatawajibu.” \p \v 19 Lakini watu wakakataa kumsikiliza Samweli wakasema, “Hapana! Tunataka mfalme wa kututawala. \v 20 Kisha tutakuwa kama mataifa mengine yote, tukiwa na mfalme wa kutuongoza na kwenda mbele yetu na kutupigania vita vyetu.” \p \v 21 Samweli aliposikia yote watu waliyosema, akarudia kuyasema mbele za Mwenyezi Mungu. \v 22 Mwenyezi Mungu akamjibu, “Wasikilize na uwape mfalme.” \p Kisha Samweli akawaambia Waisraeli, “Kila mmoja arudi mjini kwake.” \c 9 \s1 Samweli ampaka Sauli mafuta \p \v 1 Kulikuwa na Mbenyamini mmoja, mtu maarufu, ambaye aliitwa Kishi mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia wa Benyamini. \v 2 Alikuwa na mwana aliyeitwa Sauli, kijana aliyevutia sana, hakuna aliyelingana naye miongoni mwa Waisraeli; alikuwa mrefu kuliko watu wengine wote. \p \v 3 Basi punda wa Kishi baba yake Sauli walipotea, naye Kishi akamwambia mwanawe Sauli, “Mchukue mmoja wa watumishi mwende pamoja naye kuwatafuta punda.” \v 4 Hivyo akapita katika nchi ya vilima ya Efraimu na katika eneo la Shalisha, lakini hawakuwapata. Wakaendelea katika sehemu ya Shaalimu, lakini punda hawakuwa huko. Kisha wakapita katika nchi ya Benyamini, lakini hawakuwapata. \p \v 5 Walipofika sehemu ya Sufu, Sauli akamwambia mtumishi aliyekuwa pamoja naye, “Njoo turudi, au baba yangu ataacha kufikiria kuhusu punda na kuanza kufadhaika kutuhusu.” \p \v 6 Lakini mtumishi akajibu, “Tazama, katika mji huu yupo mtu wa Mungu, anayeheshimiwa sana na kila kitu asemacho kweli hutukia. Sasa na twende huko. Huenda atatuambia twende njia ipi.” \p \v 7 Sauli akamwambia mtumishi wake, “Tukienda, tutampa nini huyo mtu? Chakula kimekwisha kwenye mifuko yetu. Hatuna zawadi ya kumpelekea huyo mtu wa Mungu. Je tuna nini?” \p \v 8 Mtumishi akamjibu Sauli tena, akasema, “Tazama, nina fedha robo shekeli\f + \fr 9:8 \fr*\ft Robo shekeli ni sawa na gramu 3.\ft*\f*. Hiyo nitampa huyo mtu wa Mungu ili aweze kutuambia tutapitia njia ipi.” \v 9 (Zamani katika Israeli, kama mtu alienda kuuliza neno kwa Mungu, angesema, “Njoo na twende kwa mwonaji,” kwa sababu nabii wa sasa alikuwa akiitwa mwonaji.) \p \v 10 Sauli akamwambia mtumishi wake, “Vyema, njoo na twende.” Basi wakaenda mjini alipokuwa huyo mtu wa Mungu. \p \v 11 Walipokuwa wakipanda mlima kwenda mjini, wakakutana na baadhi ya wasichana wakikuja kuchota maji, nao wakawauliza, “Je, mwonaji yuko?” \p \v 12 Wakajibu, “Yuko, yu mbele yenu amewatangulia, sasa fanyeni haraka, ndiyo tu amekuja mjini kwetu leo, kwa kuwa watu wana dhabihu huko mahali pa juu pa kuabudia. \v 13 Mara tu mwingiapo mjini, mtamkuta kabla hajapanda kwenda mahali pa juu pa kuabudia ili kula. Watu hawataanza kula hadi atakapofika, kwa sababu ni lazima kwanza yeye abariki dhabihu, ndipo wale walioalikwa watakapokula. Pandeni sasa, mtamkuta kwa wakati huu.” \p \v 14 Wakapanda mjini, nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli alikuwa akija kuelekea walikoenda mahali pa juu pa kuabudia. \p \v 15 Basi siku moja kabla Sauli hajaja, Mwenyezi Mungu alikuwa amemfunulia Samweli jambo hili: \v 16 “Kesho wakati kama huu nitakupelekea mtu kutoka nchi ya Benyamini. Umpake mafuta awe kiongozi juu ya watu wangu Israeli; ndiye atakayewakomboa watu wangu na mkono wa Wafilisti. Nimewaangalia watu wangu, kwa kuwa kilio chao kimenifikia.” \p \v 17 Samweli alipomwona Sauli, Mwenyezi Mungu akamwambia, “Huyu ndiye mtu niliyekuambia habari zake, kwamba yeye atawatawala watu wangu.” \p \v 18 Sauli akamkaribia Samweli langoni na kumuuliza, “Tafadhali, je, unaweza kuniambia mahali nyumba ya mwonaji ilipo?” \p \v 19 Samweli akamjibu Sauli, “Mimi ndiye mwonaji, panda utangulie mbele yangu hadi mahali pa juu pa kuabudia, kwa kuwa leo itakupasa kula pamoja nami na asubuhi nitakuruhusu uende na nitakuambia yale yote yaliyo moyoni mwako. \v 20 Kuhusu wale punda uliowapoteza siku tatu zilizopita, usifadhaike kwa habari yao; wamepatikana. Ni kwa nani ambaye shauku yote ya Israeli imeelekea, kama si kwako na jamaa yote ya baba yako?” \p \v 21 Sauli akajibu, “Je, mimi si Mbenyamini, kutoka kabila dogo kuliko yote ya Israeli, nao ukoo wangu si ndio mdogo kuliko koo zote za kabila la Benyamini? Kwa nini uniambie jambo kama hili?” \p \v 22 Kisha Samweli akamleta Sauli na mtumishi wake ukumbini na kuwaketisha mahali pa heshima zaidi miongoni mwa wale waliokuwa wamealikwa; jumla yao walikuwa kama watu thelathini. \v 23 Samweli akamwambia mpishi, “Leta ile sehemu ya nyama niliyokupa, ile niliyokuambia iweke kando.” \p \v 24 Hivyo mpishi akachukua mguu pamoja na kile kilichokuwa juu yake akaiweka mbele ya Sauli. Samweli akasema, “Hiki ndicho ambacho kimewekwa kwa ajili yako. Ule, kwa sababu kilitengwa kwa ajili yako kwa tukio hili, tangu niliposema, ‘Nimewaalika wageni.’ ” Naye Sauli akala pamoja na Samweli siku ile. \p \v 25 Baada ya kushuka kutoka mahali pa juu pa kuabudia na kufika mjini, Samweli alizungumza na Sauli juu ya dari ya nyumba yake. \v 26 Walipoamka mapema alfajiri, Samweli akamwita Sauli darini, akamwambia, “Jiandae, nami nitakuaga uende zako.” Sauli alipokuwa tayari yeye na Samweli wakatoka nje pamoja. \v 27 Walipokuwa wakiteremka kuelekea mwisho wa mji, Samweli akamwambia Sauli, “Mwambie mtumishi atangulie mbele yetu.” Naye mtumishi akafanya hivyo. “Subiri hapa kidogo ili nipate kukupa ujumbe kutoka kwa Mungu.” \c 10 \p \v 1 Ndipo Samweli akachukua chupa ndogo ya mafuta na kuyamimina juu ya kichwa cha Sauli, akambusu, akisema, “Je, Mwenyezi Mungu hakukupaka mafuta uwe kiongozi juu ya urithi wake? \v 2 Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli, huko Selsa kwenye mpaka wa Benyamini. Watakuambia, ‘Punda wale uliotoka kwenda kuwatafuta, wamekwisha kupatikana. Sasa baba yako ameacha kufikiri kuhusu punda na sasa ana hofu kukuhusu wewe. Anauliza, “Nitafanyaje kuhusu mwanangu?” ’ \p \v 3 “Kisha utaenda mbele kutoka hapa hadi uufikie mwaloni wa Tabori. Watu watatu wanaopanda kwenda kumwabudu Mungu huko Betheli watakutana nawe hapo. Mmoja atakuwa amechukua wana-mbuzi watatu, mwingine mikate mitatu, na mwingine kiriba cha divai. \v 4 Watakusalimu na kukupa mikate miwili, ambayo utaipokea kutoka kwao. \p \v 5 “Baada ya hayo utaenda Gibea ya Mungu, ambapo hapo kuna kambi ya Wafilisti. Unapokaribia mji utakutana na kundi la manabii wakiteremka kutoka mahali pa juu pa kuabudia wakiwa na vinubi, matari, filimbi na zeze vikipigwa mbele yao, nao watakuwa wakitoa unabii. \v 6 Roho wa Mwenyezi Mungu atakuja juu yako kwa nguvu, nawe utatoa unabii pamoja nao; nawe utageuzwa kuwa mtu wa tofauti. \v 7 Mara ishara hizi zitakapotimizwa, fanya lolote mkono wako upasao kufanya, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe. \p \v 8 “Tangulia kushuka mbele yangu hadi Gilgali. Hakika nami nitateremka nikujie ili kutoa dhabihu za sadaka za kuteketezwa na dhabihu za amani, lakini lazima ungoje kwa siku saba hata nitakapokujia na kukuambia likupasalo kufanya.” \s1 Sauli afanywa mfalme \p \v 9 Ikawa Sauli alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu aliubadilisha moyo wa Sauli, na ishara hizi zote zikatimizwa siku ile. \v 10 Walipofika Gibea, akakutana na kundi la manabii. Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akajiunga nao katika kutoa unabii kwao. \v 11 Ikawa wale wote waliomfahamu hapo mwanzo walipomwona akitoa unabii pamoja na manabii, wakaulizana, “Ni nini hiki kilichomtokea mwana wa Kishi? Je, Sauli naye pia yumo miongoni mwa manabii?” \p \v 12 Mtu mmoja ambaye aliishi huko akajibu, “Je, naye baba yao ni nani?” Basi ikawa mithali, kusema, “Je, Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?” \v 13 Baada ya Sauli kumaliza kutoa unabii, alienda mahali pa juu pa kuabudia. \p \v 14 Basi babaye mdogo akamuuliza Sauli na mtumishi wake, “Je, mlikuwa wapi?” \p Akajibu, “Tulikuwa tukiwatafuta punda. Lakini tulipoona hawapatikani, tulienda kwa Samweli.” \p \v 15 Babaye mdogo Sauli akasema, “Niambie Samweli amekuambia nini.” \p \v 16 Sauli akajibu, “Alituhakikishia kwamba punda wamepatikana.” Lakini hakumwambia babaye mdogo kila kitu Samweli alichomwambia kuhusu ufalme. \p \v 17 Samweli akawaita watu wa Israeli kuja kwa Mwenyezi Mungu huko Mispa, \v 18 naye akawaambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Niliwatoa Israeli kutoka Misri, nami niliwaokoa toka nguvu za Misri na falme zote zilizowadhulumu.’ \v 19 Lakini sasa mmemkataa Mungu wenu, ambaye anawaokoa toka katika maafa yenu yote na taabu zenu zote. Nanyi mmesema, ‘Hapana, tuteulie mfalme atutawale.’ Sasa basi, jihudhurisheni wenyewe mbele za Mwenyezi Mungu kwa makabila yenu na kwa koo zenu.” \p \v 20 Samweli alipoyasogeza makabila yote ya Israeli, kabila la Benyamini likachaguliwa. \v 21 Kisha akalisogeza mbele kabila la Benyamini, kufuatana na koo zao, nao ukoo wa Matri ukachaguliwa. Mwishoni Sauli mwana wa Kishi akachaguliwa. Lakini walipomtafuta, hakuonekana. \v 22 Wakazidi kuuliza kwa Mwenyezi Mungu, “Je, huyo mtu amekwisha kufika hapa?” \p Naye Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, amejificha kwenye mizigo.” \p \v 23 Wakakimbia na kumleta kutoka huko, naye aliposimama kati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wengine wote. \v 24 Samweli akawaambia watu wote, “Je, mnamwona mtu ambaye Mwenyezi Mungu amemchagua? Hayupo aliye kama yeye miongoni mwa watu wote.” \p Ndipo watu wakasema kwa sauti kuu, “Mfalme aishi maisha marefu.” \p \v 25 Samweli akawaeleza watu madaraka ya ufalme. Akayaandika kwenye kitabu na kukiweka mbele za Mwenyezi Mungu. Kisha Samweli akawaruhusu watu kila mmoja aende nyumbani mwake. \p \v 26 Sauli pia akaenda nyumbani mwake huko Gibea, akisindikizwa na watu hodari ambao Mungu alikuwa amegusa mioyo yao. \v 27 Lakini baadhi ya watu wakorofi walisema, “Huyu mtu atawezaje kutuokoa?” Wakamdharau na wala hawakumletea zawadi. Lakini Sauli akakaa kimya. \c 11 \s1 Sauli aukomboa mji wa Yabeshi \p \v 1 Nahashi Mwamoni akakwea kuuzingira mji wa Yabesh-Gileadi kwa jeshi. Wanaume wote wa Yabeshi wakamwambia, “Fanya mkataba nasi, na tutakutumikia.” \p \v 2 Lakini Nahashi yule Mwamoni akajibu, “Nitafanya mkataba na ninyi tu kwa sharti kwamba nitang’oa jicho la kulia la kila mmoja wenu, na hivyo kuleta aibu juu ya Israeli yote.” \p \v 3 Viongozi wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe siku saba ili tuweze kutuma wajumbe katika Israeli yote. Ikies hakuna hata mmoja atayekuja kutuokoa, tutajisalimisha kwako.” \p \v 4 Wajumbe walipofika Gibea ya Sauli na kutoa taarifa kuhusu masharti haya kwa watu, wote walilia kwa sauti kubwa. \v 5 Wakati huo huo Sauli alikuwa anarudi kutoka mashambani, akiwa nyuma ya maksai wake, naye akauliza, “Watu wana nini? Mbona wanalia?” Ndipo wakamweleza vile wanaume wa Yabeshi walivyokuwa wamesema. \p \v 6 Sauli aliposikia maneno yao, Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akawaka hasira. \v 7 Akachukua maksai wawili na kuwakata vipande vipande, naye kuvituma hivyo vipande kupitia wajumbe katika Israeli yote, wakitangaza, “Hivi ndivyo itakavyofanyika kwa maksai wa kila mmoja ambaye hatamfuata Sauli na Samweli.” Kisha kicho cha Mwenyezi Mungu kikawaangukia watu, nao wakatoka kama mtu mmoja. \v 8 Sauli alipowakusanya huko Bezeki, wanaume wa Israeli walikuwa elfu mia tatu, na wanaume wa Yuda elfu thelathini. \p \v 9 Wakawaambia wale wajumbe waliokuwa wamekuja, “Waambieni wanaume wa Yabesh-Gileadi, ‘Kesho kabla jua halijawa kali, mtaokolewa.’ ” Wajumbe walipoenda na kutoa taarifa hii kwa wanaume wa Yabeshi, wakafurahi. \v 10 Wakawaambia Waamoni, “Kesho tutajisalimisha kwenu, nanyi mtaweza kututendea chochote mnachoona chema kwenu.” \p \v 11 Kesho yake Sauli alitenganisha watu wake katika vikosi vitatu; wakati wa zamu ya mwisho ya usiku wakaingia katika kambi ya Waamoni na kuwachinja hadi mchana. Wale walionusurika wakatawanyika, hivi kwamba hawakusalia watu wawili pamoja. \s1 Sauli athibitishwa kuwa mfalme \p \v 12 Kisha watu wakamwambia Samweli, “Ni nani yule aliyeuliza, ‘Je, Sauli atatutawala?’ Tuletee hawa watu, nasi tutawaua.” \p \v 13 Lakini Sauli akasema, “Hakuna hata mmoja atakayeuawa leo, kwa kuwa siku hii Mwenyezi Mungu ameokoa Israeli.” \p \v 14 Ndipo Samweli akawaambia watu, “Njooni, twendeni Gilgali na huko tuthibitishe ufalme.” \v 15 Kwa hiyo watu wote wakaenda Gilgali na kumthibitisha Sauli kuwa mfalme mbele za Mwenyezi Mungu. Huko wakatoa dhabihu za sadaka za amani mbele za Mwenyezi Mungu, naye Sauli na Waisraeli wote wakafanya karamu kubwa. \c 12 \s1 Hotuba ya Samweli ya kuaga \p \v 1 Samweli akawaambia Israeli wote, “Nimesikiliza kila kitu mlichoniambia nami nimewawekea mfalme juu yenu. \v 2 Sasa mnaye mfalme kama kiongozi wenu. Lakini mimi ni mzee na nina mvi, nao wanangu wapo hapa pamoja nanyi. Nimekuwa kiongozi wenu tangu ujana wangu hadi siku hii ya leo. \v 3 Mimi ninasimama hapa. Shuhudieni dhidi yangu mbele za Mwenyezi Mungu na mpakwa mafuta wake. Nimechukua maksai wa nani? Nimechukua punda wa nani? Ni nani nimepata kumdanganya? Nimemdhulumu nani? Nimepokea rushwa kutoka kwa nani ili nifumbe macho yangu? Kama nimefanya chochote katika hivi, nitawarudishia.” \p \v 4 Wakajibu, “Hujatudanganya wala kutudhulumu. Hujapokea chochote kutoka mkono wa mtu yeyote.” \p \v 5 Samweli akawaambia, “Mwenyezi Mungu ni shahidi dhidi yenu, pia mpakwa mafuta wake ni shahidi siku hii ya leo, kwamba hamkukuta chochote mkononi mwangu.” \p Wakasema, “Yeye ni shahidi.” \p \v 6 Kisha Samweli akawaambia watu, “Mwenyezi Mungu ndiye alimchagua Musa na Haruni, na kuwaleta baba zenu akiwapandisha kutoka Misri. \v 7 Sasa basi, simameni hapa, kwa sababu nitakabiliana nanyi kwa ushahidi mbele za Mwenyezi Mungu wa matendo yote ya haki yaliyofanywa na Mwenyezi Mungu kwenu na kwa baba zenu. \p \v 8 “Baada ya Yakobo kuingia Misri, walimlilia Mwenyezi Mungu awasaidie, naye Mwenyezi Mungu akawatuma Musa na Haruni, ambao waliwatoa baba zenu kutoka Misri na kuwakalisha mahali hapa. \p \v 9 “Lakini wakamsahau Mwenyezi Mungu, Mungu wao, hivyo Mungu akawauza katika mkono wa Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori na katika mikono ya Wafilisti na mfalme wa Moabu, ambaye alipigana dhidi yao. \v 10 Wakamlilia Mwenyezi Mungu na kusema, ‘Tumetenda dhambi; tumemwacha Mwenyezi Mungu na kutumikia Mabaali na Maashtorethi. Lakini sasa tuokoe kutoka mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia.’ \v 11 Ndipo Mwenyezi Mungu akawatuma Yerub-Baali\f + \fr 12:11 \fr*\ft pia aliitwa \ft*\fqa Gideoni\fqa*\f*, Baraka, Yefta na Samweli, naye akawaokoa kutoka mikononi mwa adui zenu kila upande, ili ninyi mpate kukaa salama. \p \v 12 “Lakini mlipomwona yule Nahashi mfalme wa Waamoni anakuja dhidi yenu, mliniambia, ‘Hapana, tunataka mfalme atutawale,’ hata ingawa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alikuwa mfalme wenu. \v 13 Sasa huyu hapa ndiye mfalme mliyemchagua, yule mliyeomba; tazameni, Mwenyezi Mungu amemweka mfalme juu yenu. \v 14 Mkimcha Mwenyezi Mungu, na kumtumikia na kumtii, nanyi msipoasi dhidi ya amri zake, ninyi pamoja na mfalme anayewatawala mkimfuata Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mambo yatakuwa mema kwenu! \v 15 Lakini kama hamkumtii Mwenyezi Mungu, nanyi mkaasi dhidi ya amri zake, mkono wake utakuwa dhidi yenu, kama ulivyokuwa dhidi ya baba zenu. \p \v 16 “Sasa basi, simameni kimya mkaone jambo hili kubwa ambalo Mwenyezi Mungu anaenda kulifanya mbele ya macho yenu! \v 17 Je, sasa si mavuno ya ngano? Nitamwomba Mwenyezi Mungu ili alete ngurumo na mvua. Nanyi mtatambua jambo hili lilivyo baya mlilolifanya mbele za macho ya Mwenyezi Mungu mlipoomba mfalme.” \p \v 18 Kisha Samweli akamwomba Mwenyezi Mungu, na siku ile ile Mwenyezi Mungu akatuma ngurumo na mvua. Hivyo watu wote wakamwogopa sana Mwenyezi Mungu na Samweli. \p \v 19 Watu wote wakamwambia Samweli, “Mwombe Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa ajili ya watumishi wako, ili tusije tukafa, kwa kuwa tumeongeza uovu juu ya dhambi zetu nyingine kwa kuomba mfalme.” \p \v 20 Samweli akajibu, “Msiogope, mmefanya uovu huu wote; hata hivyo msimwache Mwenyezi Mungu, bali mtumikieni Mwenyezi Mungu kwa moyo wote. \v 21 Msigeukie sanamu batili. Haziwezi kuwatendea jema, wala haziwezi kuwaokoa kwa sababu hazina maana. \v 22 Kwa ajili ya jina lake kuu Mwenyezi Mungu hatawakataa watu wake, kwa sababu ilimpendeza Mwenyezi Mungu kuwafanya watu wake mwenyewe. \v 23 Lakini iwe mbali nami kutenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu kwa kushindwa kuwaombea. Mimi nitawafundisha njia iliyo njema na nyoofu. \v 24 Lakini hakikisheni mnamcha Mwenyezi Mungu na kumtumikia kwa uaminifu kwa moyo wote; tafakarini mambo makubwa aliyoyatenda kwa ajili yenu. \v 25 Hata hivyo mkiendelea kufanya uovu, ninyi na mfalme wenu mtafutiliwa mbali!” \c 13 \s1 Samweli amkemea Sauli \p \v 1 Sauli alikuwa na umri wa miaka thelathini, alipokuwa mfalme, akatawala Israeli miaka arobaini na mbili. \p \v 2 Sauli alichagua watu elfu tatu kutoka Israeli; miongoni mwa hao, watu elfu mbili walikuwa naye huko Mikmashi na katika nchi ya vilima ya Betheli; nao watu elfu moja walikuwa na Yonathani huko Gibea ya Benyamini. Watu waliosalia aliwarudisha nyumbani mwao. \p \v 3 Yonathani akashambulia ngome ya Wafilisti huko Geba, nao Wafilisti wakapata habari hizo. Kisha Sauli akaamuru tarumbeta ipigwe nchi yote na kusema, “Waebrania na wasikie!” \v 4 Hivyo Israeli wote wakasikia habari kwamba: “Sauli ameshambulia ngome ya Wafilisti, na sasa Israeli wamekuwa harufu mbaya kwa Wafilisti.” Basi watu waliitwa kuungana na Sauli huko Gilgali. \p \v 5 Wafilisti wakakusanyika ili kupigana na Israeli, wakiwa na magari ya vita elfu tatu, waendesha magari ya vita elfu sita, na askari wa miguu wengi kama mchanga wa ufuoni mwa bahari. Walipanda na kupiga kambi huko Mikmashi, mashariki mwa Beth-Aveni. \v 6 Waisraeli walipoona kuwa hali yao ni ya hatari na kuwa jeshi lao limesongwa sana, wakajificha katika mapango na katika vichaka, katika miamba, kwenye mashimo na kwenye mahandaki. \v 7 Hata baadhi ya Waebrania wakavuka Yordani hadi nchi ya Gadi na Gileadi. \p Sauli akabaki huko Gilgali, navyo vikosi vyote vilivyokuwa pamoja naye vilikuwa vikitetemeka kwa hofu. \v 8 Akangoja kwa siku saba, muda uliowekwa na Samweli; lakini Samweli hakuja Gilgali, nao watu wa Sauli wakaanza kutawanyika. \v 9 Basi akasema, “Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani.” Naye Sauli akatoa sadaka ya kuteketezwa. \v 10 Mara alipomaliza kutoa hiyo sadaka, Samweli akatokea, naye Sauli akaondoka kwenda kumlaki. \p \v 11 Samweli akamuuliza, “Umefanya nini?” \p Sauli akajibu, “Nilipoona kwamba watu wanatawanyika, na kwamba hukuja wakati uliopangwa na kwamba Wafilisti walikuwa wakikusanyika huko Mikmashi, \v 12 nikawaza, ‘Sasa Wafilisti watateremka dhidi yangu huko Gilgali nami sijaomba kibali kwa Mwenyezi Mungu.’ Hivyo nikalazimika kutoa sadaka ya kuteketezwa.” \p \v 13 Samweli akamwambia Sauli, “Umetenda kwa upumbavu. Hukuyashika maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aliyokupa. Kama ungetii, angeudumisha ufalme wako juu ya Israeli kwa wakati wote. \v 14 Lakini sasa ufalme wako hautadumu; Mwenyezi Mungu amemtafuta mtu aupendezaye moyo wake, na amemchagua awe kiongozi wa watu wake, kwa sababu hukuyatii maagizo ya Mwenyezi Mungu.” \p \v 15 Kisha Samweli akaondoka Gilgali, akapanda Gibea ya Benyamini, naye Sauli akawahesabu watu aliokuwa nao. Jumla yao walikuwa watu mia sita. \s1 Israeli bila silaha \p \v 16 Sauli, mwanawe Yonathani na watu waliokuwa pamoja nao walikuwa wakiishi huko Gibea ya Benyamini, wakati Wafilisti wakiwa wamepiga kambi huko Mikmashi. \v 17 Makundi ya wavamiaji walikuja kutoka kambi ya Wafilisti katika vikosi vitatu. Kikosi kimoja kilielekea Ofra karibu na Shuali, \v 18 kikosi kingine kilielekea Beth-Horoni, nacho kikosi cha tatu kilielekea kwenye nchi ya mpakani ielekeayo Bonde la Seboimu linalotazamana na jangwa. \p \v 19 Hapakuwa na mhunzi ambaye angeweza kupatikana katika nchi yote ya Israeli, kwa sababu Wafilisti walikuwa wamesema, “Waebrania wasije wakatengeneza panga au mikuki!” \v 20 Hivyo Waisraeli wote waliteremka kwa Wafilisti ili kila mtu kunoa plau yake, jembe lake, shoka lake, au mundu wake. \v 21 Bei ilikuwa fedha theluthi mbili za shekeli\f + \fr 13:21 \fr*\ft Theluthi mbili za shekeli za fedha ni sawa na gramu 8.\ft*\f* kunoa majembe ya plau na majembe ya mkono, na theluthi moja ya shekeli\f + \fr 13:21 \fr*\ft Theluthi moja ya shekeli ya fedha ni sawa na gramu 4.\ft*\f* kunoa uma, na shoka, na mchokoo. \p \v 22 Kwa hiyo siku ya vita hakuna askari yeyote kambini na Sauli na Yonathani aliyekuwa na upanga wala mkuki mkononi mwake; Sauli na mwanawe Yonathani tu ndio walikuwa navyo. \s1 Yonathani awashambulia Wafilisti \p \v 23 Basi kikosi cha Wafilisti kilikuwa kimetoka kuelekea njia iendayo Mikmashi. \c 14 \nb \v 1 Siku moja Yonathani mwana wa Sauli akamwambia kijana mbeba silaha wake, akasema, “Njoo, tuwavukie Wafilisti kwenye doria upande ule mwingine.” Lakini hakumwambia baba yake. \p \v 2 Sauli alikuwa akikaa kwenye viunga vya Gibea chini ya mkomamanga huko Migroni. Alikuwa pamoja na watu wapatao mia sita; \v 3 miongoni mwao alikuwepo Ahiya, aliyekuwa amevaa kizibau. Alikuwa mwana wa Ikabodi, nduguye Ahitubu mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Mwenyezi Mungu huko Shilo. Hakuna yeyote aliyekuwa na habari kwamba Yonathani alikuwa ameondoka. \p \v 4 Kila upande wa njia ambayo Yonathani alikusudia kupita ili kuvuka kufikia doria ya Wafilisti kulikuwa na jabali; moja lilikuwa linaitwa Bosesi, na jingine Sene. \v 5 Jabali moja lilisimama kaskazini kuelekea Mikmashi na jingine upande wa kusini kuelekea Geba. \p \v 6 Yonathani akamwambia kijana wake mbeba silaha, “Njoo, tuvukie doria ya wale jamaa wasiotahiriwa. Huenda Mwenyezi Mungu atatenda kwa ajili yetu. Hakuna chochote kitakachoweza kumzuia Mwenyezi Mungu kuokoa, kwamba ni kwa wingi au kwa uchache.” \p \v 7 Mbeba silaha wake akamwambia, “Fanya yale yote uliyo nayo katika moyo wako. Songa mbele; moyo wangu na roho yangu viko pamoja nawe.” \p \v 8 Yonathani akasema, “Basi njoo; tutavuka kuwaelekea hao watu na kuacha watuone. \v 9 Wakituambia, ‘Subirini hapo hadi tuje kwenu,’ tutakaa pale tulipo na hatutakwea kwao. \v 10 Lakini kama watasema, ‘Pandeni mje kwetu,’ tutakwea, kwa sababu hiyo itakuwa ishara yetu kwamba Mwenyezi Mungu amewatia mikononi mwetu.” \p \v 11 Basi wote wawili wakajionesha kwa doria ya Wafilisti. Wafilisti wakasema, “Tazama! Waebrania wanatambaa toka mashimoni walimokuwa wamejificha.” \v 12 Wanaume wa kwenye doria wakawapazia sauti Yonathani na mbeba silaha wake, wakisema, “Njooni, pandeni kwetu, nasi tutawakomesha.” \p Basi Yonathani akamwambia mbeba silaha wake, “Panda nyuma yangu; Mwenyezi Mungu amewatia mikononi mwa Israeli.” \p \v 13 Yonathani akapanda juu, akitumia mikono yake na miguu, pamoja na mbeba silaha wake papo hapo nyuma yake. Wafilisti wakaanguka mbele ya Yonathani, naye mbeba silaha wake akamfuata akiwaua nyuma yake. \v 14 Katika hilo shambulio la kwanza, Yonathani na mbeba silaha wake waliua kama watu ishirini kwenye eneo kama la nusu eka. \s1 Waisraeli wafukuza Wafilisti \p \v 15 Kisha fadhaa ikawapata jeshi lote, wale waliokuwa kambini na shambani, wale waliokuwa katika doria na makundi ya washambuliaji, nayo ardhi ilitetemeka. Ilikuwa ni hofu ya ghafula iliyotumwa na Mungu. \p \v 16 Wapelelezi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaona jeshi likitokomea pande zote. \v 17 Ndipo Sauli akawaambia watu wale waliokuwa pamoja naye, “Kagueni jeshi mkaone ni nani ameondoka kwetu.” Walipokagua, akawa ni Yonathani na mbeba silaha wake ambao hawakuwepo. \p \v 18 Sauli akamwambia Ahiya, “Leta Sanduku la Mungu.” (Wakati huo lilikuwa kwa Waisraeli.) \v 19 Sauli alipokuwa akisema na kuhani, makelele katika kambi ya Wafilisti yakaongezeka zaidi na zaidi. Hivyo Sauli akamwambia kuhani, “Rudisha mkono wako.” \p \v 20 Kisha Sauli na watu wake wote wakakusanyika na kwenda vitani. Wakawakuta Wafilisti wakiwa wamechanganyikiwa kabisa, wakitiana panga kila mmoja na wenzake. \v 21 Wale Waebrania ambao walishakuwa pamoja na Wafilisti, na waliokuwa wamepanda pamoja nao katika kambi zao, wakaenda upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani. \v 22 Waisraeli wote waliokuwa wamejificha katika nchi ya vilima ya Efraimu waliposikia kuwa Wafilisti wamekimbia, wakajiunga vitani na kuwafuata kwa bidii. \v 23 Hivyo Mwenyezi Mungu akawaokoa Waisraeli siku ile, navyo vita vilienea hadi kupita Beth-Aveni. \s1 Yonathani ala Asali \p \v 24 Basi Waisraeli walikuwa katika dhiki siku ile, kwa sababu Sauli alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, akisema, “Alaaniwe mtu yeyote atakayekula chakula kabla ya jioni, kabla sijalipiza kisasi juu ya adui zangu!” Kwa hiyo hakuna mtu yeyote katika jeshi aliyeonja chakula. \p \v 25 Jeshi lote liliingia mwituni, na huko kulikuwa na asali juu ya ardhi. \v 26 Walipoingia mwituni, wakaona asali ikitiririka, hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyetia mkono wake kinywani, kwa sababu waliogopa kiapo. \v 27 Lakini Yonathani alikuwa hajasikia kuwa baba yake alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, hivyo akainyoosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake na kuichovya katika sega la asali. Akainua mkono wake na kuutia kinywani mwake, nayo macho yake yakaangaa. \v 28 Kisha mmoja wa askari wake akamwambia, “Baba yako alilifunga jeshi kwa kiapo kikali, akisema, ‘Alaaniwe mtu yeyote alaye chakula leo!’ Ndiyo sababu watu wanalegea.” \p \v 29 Yonathani akasema, “Baba yangu ameitaabisha nchi. Ona jinsi macho yangu yalipata kuangaa nilipoonja asali hii kidogo. \v 30 Ingekuwa bora zaidi mara ngapi kama watu wangekula leo baadhi ya nyara walizoteka kutoka kwa adui zao. Je, mauaji ya Wafilisti yasingekuwa makubwa zaidi?” \p \v 31 Siku ile baada ya Waisraeli kuwaua Wafilisti kutoka Mikmashi hadi Aiyaloni, walikuwa wamechoka. \v 32 Watu wakarukia zile nyara, wakichukua kondoo, ng’ombe na ndama, wakawachinja hapo juu ya nchi na kuwala, pamoja na damu. \v 33 Kisha mtu mmoja akamwambia Sauli, “Tazama, watu wanatenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu kwa kula nyama yenye damu.” \p Akasema, “Mmevunja uaminifu. Livingirisheni jiwe kubwa hapa mara moja.” \v 34 Kisha Sauli akasema, “Nendeni miongoni mwa watu, mwaambie, ‘Kila mmoja wenu aniletee ng’ombe wake na kondoo, mwachinjie hapa na mle. Msitende dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu kwa kula nyama ikiwa na damu ndani yake.’ ” \p Hivyo kila mmoja akaleta ng’ombe wake jioni ile na kumchinja hapo. \v 35 Ndipo Sauli akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu, na ndiyo ilivyokuwa mara yake ya kwanza kujenga madhabahu. \p \v 36 Sauli akasema, “Tuteremke tufuatie Wafilisti usiku na kuwateka nyara hadi mapambazuko, nasi tusiache hata mmoja wao hai.” \p Wakajibu, “Fanya lolote lile uonalo jema zaidi kwako.” \p Lakini kuhani akasema, “Tuulize kwa Mungu mahali hapa.” \p \v 37 Basi Sauli akamuuliza Mungu, akisema, “Je, niteremke kuwafuatia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Israeli?” Lakini Mungu hakumjibu siku ile. \p \v 38 Kwa hiyo Sauli akasema, “Njooni hapa, ninyi nyote ambao ni viongozi wa jeshi, na tutafute ni dhambi gani imefanywa leo. \v 39 Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aiokoaye Israeli aishivyo, hata kama itakuwa kwa mwana wangu Yonathani, ni lazima afe.” Lakini hakuna mtu yeyote aliyesema neno. \p \v 40 Kisha Sauli akawaambia Waisraeli wote, “Ninyi simameni huko; mimi na mwanangu Yonathani tutasimama hapa.” \p Watu wakajibu, “Fanya lile unaloona jema zaidi kwako.” \p \v 41 Kisha Sauli akamwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, akisema, “Kwa nini hujamjibu mtumishi wako leo? Ikiwa makosa ni yangu au ya mwanangu Yonathani, jibu kwa Urimu. Lakini ikiwa makosa ni ya wanaume wa Israeli, jibu kwa Thumimu.”\f + \fr 14:41 \fr*\ft Maandiko ya Kiebrania hayana maneno: “Kwa nini … Thumimu.” Yana maneno: \ft*\fqa “Nipe jibu lililo sawa.”\fqa*\f* Yonathani na Sauli wakatolewa kwa kura, nao watu wakawa salama. \v 42 Sauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Kura ikamwangukia Yonathani. \p \v 43 Basi Sauli akamwambia Yonathani, “Niambie ni nini ulichokifanya.” \p Hivyo Yonathani akamwambia, “Nilionja tu asali kidogo kwa ncha ya fimbo yangu. Je, sasa ni lazima nife?” \p \v 44 Sauli akasema, “Mungu na aniadhibu vikali zaidi kama wewe Yonathani hutakufa.” \p \v 45 Lakini watu wakamwambia Sauli, “Je, Yonathani atakufa, yeye ambaye ameleta ukombozi huu mkubwa kwa Israeli? Hasha! Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, hakuna hata unywele wa kichwa chake utakaoanguka juu ya ardhi, kwa kuwa alifanya jambo hili leo kwa msaada wa Mungu.” Basi watu wakamwokoa Yonathani, wala hakuuawa. \p \v 46 Kisha Sauli akaacha kuwafuata Wafilisti, nao wakajiondoa na kurudi katika nchi yao. \p \v 47 Baada ya Sauli kujitwalia utawala katika Israeli, alipigana dhidi ya adui zake kila upande: Moabu, Waamoni, Edomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Popote alipogeukia, aliwashinda. \v 48 Akapigana kishujaa na kuwashinda Waamaleki, akiikomboa Israeli kutoka mikono ya wale waliokuwa wamewateka nyara. \s1 Jamaa ya Sauli \p \v 49 Wana wa Sauli walikuwa Yonathani, Ishvi na Malki-Shua. Jina la binti yake mkubwa lilikuwa Merabu, naye mdogo aliitwa Mikali. \v 50 Jina la mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu binti Ahimaasi. Jina la jemadari wa jeshi la Sauli aliitwa Abneri mwana wa Neri, naye Neri alikuwa babaye mdogo Sauli. \v 51 Babaye Sauli, yaani Kishi, na Neri baba yake Abneri walikuwa wana wa Abieli. \p \v 52 Siku zote za utawala wa Sauli zilikuwa za vita vikali dhidi ya Wafilisti, na wakati wowote Sauli alimwona mtu mwenye nguvu au shujaa, alimchukua kwa utumishi wake. \c 15 \s1 Mwenyezi Mungu amkataa Sauli \p \v 1 Samweli akamwambia Sauli, “Mimi ndiye Mwenyezi Mungu alinituma nikupake mafuta ili uwe mfalme juu ya watu wake Israeli; basi sasa sikiliza ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu. \v 2 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Nitawaadhibu Waamaleki kwa kile walichowatendea Israeli walipowavizia wakati walipanda kutoka Misri. \v 3 Basi sasa nenda ukawashambulie Waamaleki na kuwaangamiza kabisa pamoja na kila kitu kilicho mali yao. Usiwahurumie; waue wanaume na wanawake, watoto na wale wanaonyonya, ng’ombe na kondoo, ngamia na punda.’ ” \p \v 4 Ndipo Sauli akawaita watu na kuwapanga huko Telaimu, askari wa miguu elfu mia mbili, na elfu kumi kutoka Yuda. \v 5 Sauli akaenda katika mji wa Amaleki na kuwavizia bondeni. \v 6 Kisha akawaambia Wakeni, “Ondokeni, waacheni Waamaleki ili nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao, kwa kuwa ninyi mliwatendea mema Waisraeli wote wakati walipanda kutoka Misri.” Basi Wakeni wakaondoka, wakawaacha Waamaleki. \p \v 7 Ndipo Sauli akawashambulia Waamaleki toka Havila hadi Shuri, mashariki mwa Misri. \v 8 Akamchukua Agagi mfalme wa Waamaleki akiwa hai, nao watu wake wote akawaangamiza kabisa kwa upanga. \v 9 Lakini Sauli na hilo jeshi wakamhifadhi hai Agagi, na kondoo na ng’ombe walio wazuri, mafahali na wana-kondoo walionona, na kila kitu kilichokuwa kizuri. Hivi vitu hawakuwa radhi kuviangamiza kabisa, bali kila kitu kilichodharauliwa na kilicho dhaifu wakakiangamiza kabisa. \p \v 10 Kisha neno la Mwenyezi Mungu likamjia Samweli kusema: \v 11 “Ninasikitika kwamba nimemfanya Sauli kuwa mfalme, kwa sababu ameacha kunifuata mimi na hakutimiza maagizo yangu.” Samweli akafadhaika, naye akamlilia Mwenyezi Mungu usiku ule wote. \p \v 12 Asubuhi na mapema Samweli akaamka kwenda kukutana na Sauli, lakini akaambiwa, “Sauli ameenda Karmeli. Huko amesimamisha mnara kwa heshima yake mwenyewe, naye ameendelea na kuteremkia Gilgali.” \p \v 13 Samweli alipomfikia, Sauli akamwambia, “Mwenyezi Mungu akubariki! Nimetimiza yale Mwenyezi Mungu aliyoniagiza.” \p \v 14 Lakini Samweli akasema, “Nini basi huu mlio wa kondoo masikioni mwangu? Huu mlio wa ng’ombe ninaousikia ni kitu gani?” \p \v 15 Sauli akajibu, “Askari wamewaleta kutoka kwa Waamaleki, waliwaacha wale kondoo na ng’ombe wazuri ili kuwatoa dhabihu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, lakini tuliwaangamiza kabisa wengine wote.” \p \v 16 Samweli akamwambia Sauli, “Ngoja! Nami nitakuambia lile Mwenyezi Mungu aliloniambia usiku huu.” \p Sauli akajibu, “Niambie.” \p \v 17 Samweli akamwambia, “Ingawa zamani ulijiona mdogo machoni pako mwenyewe, Je, hukuwa kiongozi wa makabila ya Israeli? Mwenyezi Mungu alikupaka mafuta kuwa mfalme juu ya Israeli. \v 18 Naye akakutuma kwa kazi maalum, akisema, ‘Nenda ukaangamize kabisa wale watu waovu, wale Waamaleki, upigane nao vita hadi utakapowaangamiza kabisa.’ \v 19 Kwa nini hukumtii Mwenyezi Mungu? Kwa nini ulivamia nyara na kufanya uovu machoni pa Mwenyezi Mungu?” \p \v 20 Sauli akasema, “Lakini nilimtii Mwenyezi Mungu. Nilikamilisha ile kazi ambayo Mwenyezi Mungu alinituma. Niliwaangamiza Waamaleki kabisa na kumleta Agagi mfalme wao. \v 21 Askari walichukua kondoo na ng’ombe kutoka nyara, kutoka kwa wale wazuri sana katika vitu vilivyotengewa Mungu, ili wavitoe kuwa dhabihu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, huko Gilgali.” \p \v 22 Lakini Samweli akajibu: \q1 “Je, Mwenyezi Mungu anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu \q2 kama vile kuitii sauti ya Mwenyezi Mungu? \q1 Kutii ni bora kuliko dhabihu, \q2 nako kusikia ni bora \q2 kuliko mafuta ya kondoo dume. \q1 \v 23 Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya uaguzi, \q2 nao ukaidi ni kama uovu wa kuabudu sanamu. \q1 Kwa sababu umelikataa neno la Mwenyezi Mungu, \q2 naye amekukataa wewe \q2 kuendelea kuwa mfalme.” \p \v 24 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Nimetenda dhambi. Nimevunja amri ya Mwenyezi Mungu na maagizo yako. Niliwaogopa watu na kwa hiyo nikafanya walivyotaka. \v 25 Sasa ninakusihi usamehe dhambi yangu, nawe urudi pamoja nami, ili nipate kumwabudu Mwenyezi Mungu.” \p \v 26 Lakini Samweli akamwambia, “Sitarudi pamoja nawe. Umelikataa neno la Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu amekukataa wewe, usiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli!” \p \v 27 Samweli alipogeuka ili aondoke, Sauli akang’ang’ania pindo la joho lake, nalo likararuka. \v 28 Samweli akamwambia, “Mwenyezi Mungu ameurarua ufalme wa Israeli kutoka kwako leo, naye ameutia kwa mmoja wa majirani zako, aliye bora kuliko wewe. \v 29 Yeye aliye Utukufu wa Israeli hasemi uongo wala hana kigeugeu; kwa kuwa yeye si mwanadamu, hata abadili nia yake.” \p \v 30 Sauli akajibu, “Nimetenda dhambi. Lakini tafadhali niheshimu mbele ya wazee wa watu wangu na mbele ya Israeli; rudi pamoja nami, ili nipate kumwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wako.” \v 31 Hivyo Samweli akarudi pamoja na Sauli, naye Sauli akamwabudu Mwenyezi Mungu. \p \v 32 Ndipo Samweli akasema, “Niletee Agagi mfalme wa Waamaleki.” \p Agagi akaja kwake kwa ujasiri, akifikiri, “Hakika uchungu wa mauti umepita.” \p \v 33 Lakini Samweli akasema, \q1 “Kama upanga wako ulivyofanya wanawake \q2 kufiwa na watoto wao, \q1 ndivyo mama yako atakavyokuwa \q2 hana mtoto miongoni mwa wanawake.” \m Naye Samweli akamuua Agagi mbele za Mwenyezi Mungu huko Gilgali. \p \v 34 Kisha Samweli akaenda Rama, lakini Sauli akapanda nyumbani mwake huko Gibea ya Sauli. \v 35 Hadi siku Samweli alipofariki hakuenda kumwona Sauli tena, ingawa Samweli alimwomboleza. Naye Mwenyezi Mungu alihuzunika kwamba alimfanya Sauli kuwa mfalme juu ya Israeli. \c 16 \s1 Samweli ampaka Daudi mafuta \p \v 1 Mwenyezi Mungu akamwambia Samweli, “Utamlilia Sauli hadi lini, maadamu nimemkataa asiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli? Jaza pembe yako mafuta, ushike njia uende; ninakutuma kwa Yese huko Bethlehemu. Nimemchagua mmoja wa wanawe kuwa mfalme.” \p \v 2 Lakini Samweli akasema, “Nitaendaje? Sauli atasikia kuhusu jambo hili na ataniua.” \p Mwenyezi Mungu akamwambia, “Chukua ndama jike, useme, ‘Nimekuja kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu.’ \v 3 Mwalike Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonesha utakalofanya. Utanipakia mafuta yule nitakuonesha.” \p \v 4 Samweli akafanya kile Mwenyezi Mungu alichosema. Alipofika Bethlehemu, wazee wa mji wakatetemeka walipomlaki. Wakauliza, “Je, umekuja kwa amani?” \p \v 5 Samweli akajibu, “Ndiyo, kwa amani; nimekuja kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu. Jiwekeni wakfu na mje kwenye dhabihu pamoja nami.” Ndipo akamweka Yese wakfu pamoja na wanawe na kuwaalika kwenye dhabihu. \p \v 6 Walipofika, Samweli akamwona Eliabu, naye akafikiri, “Hakika mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu anasimama hapa mbele za Mwenyezi Mungu.” \p \v 7 Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia Samweli, “Usitazame sura yake wala kimo chake, kwa kuwa nimemkataa. Mwenyezi Mungu hatazami katika vile vitu mwanadamu avitazamavyo. Mwanadamu hutazama katika sura ya nje, lakini Mwenyezi Mungu hutazama moyoni.” \p \v 8 Kisha Yese akamwita Abinadabu na kumpitisha mbele ya Samweli. Lakini Samweli akasema, “Hata huyu Mwenyezi Mungu hakumchagua.” \v 9 Kisha Yese akampitisha Shama, lakini Samweli akasema, “Wala huyu Mwenyezi Mungu hakumchagua.” \v 10 Yese alikuwa na wana saba aliowapitisha mbele ya Samweli, lakini Samweli akamwambia, “Mwenyezi Mungu hajawachagua hawa.” \v 11 Hivyo akamuuliza Yese, “Je, hawa ndio wana pekee ulio nao?” \p Yese akajibu, “Bado yuko mdogo kuliko wote, lakini anachunga kondoo.” \p Samweli akasema, “Tuma aitwe; hatutaketi hadi afike.” \p \v 12 Basi akatuma aitwe, naye akaletwa. Aling’aa kwa afya, na mwenye sura nzuri na umbo la kupendeza. \p Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “Inuka na umpake mafuta; huyu ndiye.” \p \v 13 Basi Samweli akachukua ile pembe ya mafuta na kumpaka mafuta mbele ya ndugu zake. Kuanzia siku ile na kuendelea Roho wa Mwenyezi Mungu akaja juu ya Daudi kwa nguvu. Kisha Samweli akaenda zake Rama. \s1 Daudi katika utumishi kwa Sauli \p \v 14 Basi Roho wa Mwenyezi Mungu alikuwa ameondoka kwa Sauli, nayo roho mbaya ikaachiwa nafasi na Mwenyezi Mungu ili imtese. \p \v 15 Watumishi wa Sauli wakamwambia, “Tazama, roho mbaya imeachiwa nafasi na Mwenyezi Mungu nayo inakutesa. \v 16 Basi bwana wetu na aamuru watumishi wake walio hapa watafute mtu anayeweza kupiga kinubi. Atakipiga kinubi wakati roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikujiapo, nawe utajisikia vizuri.” \p \v 17 Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Mtafuteni mtu apigaye kinubi vizuri mkamlete kwangu.” \p \v 18 Mmoja wa watumishi wake akajibu, “Nimemwona mwana wa Yese Mbethlehemu ambaye anajua kupiga kinubi. Yeye ni mtu hodari na shujaa. Ni mwenye busara katika kunena, mtu mzuri wa umbo. Mwenyezi Mungu yu pamoja naye.” \p \v 19 Ndipo Sauli akatuma wajumbe kwa Yese na kumwambia, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.” \v 20 Kwa hiyo Yese akamchukua punda aliyepakizwa mikate, kiriba cha divai na mwana-mbuzi, na kuvipeleka vitu hivyo kwa Sauli pamoja na Daudi mwanawe. \p \v 21 Daudi akafika kwa Sauli na kuingia kwenye kazi yake. Sauli akampenda sana, naye Daudi akawa mmoja wa wabeba silaha wake. \v 22 Basi Sauli akatuma ujumbe kwa Yese, akisema, “Mruhusu Daudi abaki katika utumishi wangu, kwa kuwa ninapendezwa naye.” \p \v 23 Kila mara roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ilipomjia Sauli, Daudi alichukua kinubi chake na kupiga. Ndipo Sauli angetulizwa na kujisikia vizuri, nayo ile roho mbaya ingemwacha. \c 17 \s1 Daudi na Goliathi \p \v 1 Wakati huo Wafilisti wakakusanya majeshi yao kwa ajili ya vita, nao wakakusanyika huko Soko katika Yuda. Wakapiga kambi huko Efes-Damimu, kati ya Soko na Azeka. \v 2 Sauli na Waisraeli wakakusanyika na kupiga kambi katika Bonde la Ela na kupanga jeshi ili kupigana vita na Wafilisti. \v 3 Wafilisti wakawa katika kilima kimoja, na Waisraeli katika kilima kingine, nalo bonde likiwa kati yao. \p \v 4 Shujaa aliyeitwa Goliathi, aliyetoka Gathi, akajitokeza kutoka kambi ya Wafilisti. Alikuwa na urefu dhiraa sita na shibiri moja\f + \fr 17:4 \fr*\ft Dhiraa sita na shibiri moja ni sawa na mita 3.\ft*\f*. \v 5 Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani mwake, na alivaa dirii ya shaba kifuani mwake yenye uzito wa shekeli elfu tano\f + \fr 17:5 \fr*\ft Shekeli 5,000 ni sawa na kilo 58.\ft*\f*. \v 6 Miguuni mwake alivaa mabamba ya shaba, na alikuwa na mkuki wa shaba mgongoni mwake. \v 7 Mpini wa huo mkuki ulikuwa kama mti wa mfumaji, na ncha ya chuma yake ilikuwa na uzito wa shekeli mia sita\f + \fr 17:7 \fr*\ft Shekeli 600 ni sawa na kilo 7.\ft*\f*. Mbeba ngao wake alitangulia mbele yake. \p \v 8 Goliathi alisimama na kuwaambia majeshi ya Israeli kwa sauti kuu, akisema, “Kwa nini mmetoka kupanga vita? Je, mimi si Mfilisti, na ninyi ni watumishi wa Sauli? Chagueni mtu na anishukie mimi. \v 9 Kama anaweza kupigana nami na kuniua, tutakuwa chini yenu; lakini nikimshinda na kumuua, ninyi mtakuwa chini yetu, na mtatutumikia.” \v 10 Kisha yule Mfilisti akasema, “Siku hii ya leo nayatukana majeshi ya Israeli! Nipeni mtu tupigane.” \v 11 Kwa kusikia maneno ya Wafilisti, Sauli na Waisraeli wote wakafadhaika na kuogopa. \p \v 12 Basi Daudi alikuwa mwana wa Mwefrathi jina lake Yese aliyekuwa ametoka Bethlehemu ya Yuda. Yese alikuwa na wana wanane, naye wakati wa Sauli alikuwa mzee sana. \v 13 Wana wakubwa watatu wa Yese walikuwa wamefuatana na Sauli vitani: Mzaliwa wa kwanza alikuwa Eliabu, wa pili Abinadabu, na wa tatu Shama. \v 14 Daudi ndiye alikuwa mdogo wa wote. Hao wakubwa watatu wakamfuata Sauli, \v 15 lakini Daudi alikuwa akienda kwa Sauli na kurudi ili kuchunga kondoo wa baba yake huko Bethlehemu. \p \v 16 Kwa siku arobaini huyo Mfilisti alikuwa akija mbele kila siku asubuhi na jioni na kujionesha. \p \v 17 Wakati huo Yese akamwambia mwanawe Daudi, “Chukua hii efa\f + \fr 17:17 \fr*\ft Efa moja ni sawa na kilo 22.\ft*\f* ya bisi na hii mikate kumi kwa ajili ya ndugu zako uwapelekee upesi kambini mwao. \v 18 Chukua pamoja na hizi jibini kumi kwa jemadari wa kikosi chao. Ujue hali ya ndugu zako na uniletee taarifa za uhakika kutoka kwao. \v 19 Wao wako pamoja na Sauli na wanaume wote wa Israeli huko kwenye Bonde la Ela, wakipigana na Wafilisti.” \p \v 20 Asubuhi na mapema Daudi akaondoka, akaliacha kundi la kondoo pamoja na mchungaji, akapakia vitu vile na kuondoka, kama vile Yese alivyokuwa amemwagiza. Akafika kambini wakati jeshi lilikuwa likitoka kwenda kwenye sehemu yake ya kupigania, huku wakipiga ukelele wa vita. \v 21 Israeli na Wafilisti walikuwa wakipanga safu zao wakitazamana. \v 22 Daudi akaacha vile vitu vyake kwa mtunza vifaa, akakimbilia katika safu za vita na kuwasalimu ndugu zake. \v 23 Alipokuwa akisema nao, Goliathi, yule Mfilisti shujaa kutoka Gathi, akajitokeza mbele ya safu zake na kupiga ile kelele yake ya kawaida ya matukano, naye Daudi akayasikia. \v 24 Waisraeli walipomwona yule mtu, wote wakamkimbia kwa woga mkuu. \p \v 25 Basi Waisraeli walikuwa wakisema, “Je, mnaona jinsi mtu huyu anavyoendelea kujitokeza. Hujitokeza ili kutukana Israeli. Mfalme atatoa utajiri mwingi kwa yule mtu atakayemuua. Pia atamwoza binti yake na atasamehe jamaa ya baba yake kulipa kodi katika Israeli.” \p \v 26 Daudi akauliza watu waliokuwa wamesimama karibu naye, “Je, atatendewa nini mtu atakayemuua huyu Mfilisti na kuondoa aibu hii katika Israeli? Ni nani huyu Mfilisti asiyetahiriwa hata atukane majeshi ya Mungu aliye hai?” \p \v 27 Wakarudia yale yaliyokuwa yamesemwa na kumwambia kuwa, “Hili ndilo atakalotendewa mtu yule atakayemuua.” \p \v 28 Eliabu nduguye mkubwa Daudi alipomsikia akizungumza na watu hasira ikawaka juu yake akamuuliza, “Kwa nini umeteremka kuja hapa? Nao wale kondoo wachache kule nyikani umewaacha na nani? Ninajua jinsi ulivyo na kiburi na jinsi moyo wako ulivyo mwovu; umekuja hapa kutazama vita tu.” \p \v 29 Daudi akasema, “Sasa nimefanya nini? Je, siwezi hata kuongea.” \v 30 Daudi akamgeukia mtu mwingine na kumuuliza jambo lilo hilo, nao watu wakamjibu vilevile kama mwanzo. \v 31 Lile Daudi alilosema likasikiwa na kuelezwa kwa Sauli, naye Sauli akatuma aitwe. \p \v 32 Daudi akamwambia Sauli, “Mtu yeyote asife moyo kwa habari ya huyu Mfilisti; mtumishi wako ataenda kupigana naye.” \p \v 33 Sauli akamjibu Daudi, “Wewe hutaweza kwenda kupigana dhidi ya huyu Mfilisti; wewe ni kijana tu, naye amekuwa mtu wa vita tangu ujana wake.” \p \v 34 Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mtumishi wako amekuwa akichunga kondoo wa baba yake. Simba au dubu alipokuja na kuchukua kondoo kutoka kundi, \v 35 nilifuatia, nikampiga na nikampokonya kondoo kwenye kinywa chake. Aliponigeukia, nilimkamata nywele zake, nikampiga na kumuua. \v 36 Mtumishi wako ameshaua simba na dubu pia; huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wa hao, kwa sababu ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai. \v 37 Mwenyezi Mungu ambaye aliniokoa toka katika makucha ya simba na makucha ya dubu ataniokoa kutoka mikono ya huyu Mfilisti.” \p Sauli akamwambia Daudi, “Nenda, naye Mwenyezi Mungu na awe pamoja nawe.” \p \v 38 Ndipo Sauli akamvika Daudi silaha zake mwenyewe za vita. Akamvika dirii na chapeo ya shaba kichwani mwake. \v 39 Daudi akajifunga upanga juu ya hayo mavazi na kujaribu kutembea kwa sababu alikuwa hana uzoefu navyo. \p Daudi akamwambia Sauli, “Siwezi kwenda nikiwa nimevaa hivi, kwa sababu sina uzoefu navyo.” Hivyo akavivua. \v 40 Kisha akachukua fimbo yake mkononi, akachagua mawe laini matano katika kijito, akayaweka kwenye kifuko ndani ya mfuko wake wa kichungaji, akiwa na kombeo yake mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti. \p \v 41 Wakati ule ule, yule Mfilisti, akiwa na mbeba ngao wake mbele yake, akaendelea kujongea karibu na Daudi. \v 42 Mfilisti akamwangalia Daudi kote na kumwona kuwa ni kijana tu, mwekundu na mzuri wa kupendeza, naye akamdharau. \v 43 Akamwambia Daudi, “Je, mimi ni mbwa, hata unanijia na fimbo?” Yule Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. \v 44 Tena Mfilisti akamwambia, “Njoo hapa, nami nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni nyama yako.” \p \v 45 Daudi akamwambia yule Mfilisti. “Wewe unanijia na upanga, mkuki na fumo, lakini mimi ninakujia kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa majeshi ya Israeli, ambaye wewe umemtukana. \v 46 Siku hii Mwenyezi Mungu atakutia mkononi mwangu, nami nitakupiga na kukukata kichwa chako. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya jeshi la Wafilisti, nayo dunia yote itajua kuwa yuko Mungu katika Israeli. \v 47 Wale wote waliokusanyika hapa watajua kuwa Mwenyezi Mungu haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; kwa kuwa vita ni vya Mwenyezi Mungu, naye atawatia ninyi wote mikononi mwetu.” \p \v 48 Yule Mfilisti aliposogea karibu ili kumshambulia, Daudi akaenda mbio kuelekea safu ya vita kukutana naye. \v 49 Daudi akatia mkono wake mfukoni na kuchukua jiwe, akalirusha kwa kombeo, nalo likampiga yule Mfilisti kwenye paji la uso. Lile jiwe likaingia kipajini mwa uso, akaanguka kifudifudi. \p \v 50 Basi Daudi akamshinda huyo Mfilisti kwa kombeo na jiwe; bila kuwa na upanga mkononi mwake akampiga huyo Mfilisti na kumuua. \p \v 51 Daudi akakimbia na kusimama juu yake. Akaushika upanga wa huyo Mfilisti na kuuvuta toka kwenye ala yake. Baada ya kumuua, akakata kichwa chake kwa ule upanga. \p Wafilisti walipoona kuwa shujaa wao amekufa, wakageuka na kukimbia. \v 52 Ndipo wanaume wa Israeli na Yuda wakainuka kwenda mbele wakipiga kelele na kufuatia Wafilisti hadi kwenye ingilio la Gathi kwenye malango ya Ekroni. Maiti zao zilitawanyika kando ya barabara ya Shaaraimu hadi Gathi na Ekroni. \v 53 Waisraeli waliporudi kutoka kuwafukuza Wafilisti, waliteka nyara kutoka kambi yao. \v 54 Daudi akachukua kichwa cha yule Mfilisti na kukileta Yerusalemu, naye akaweka silaha za huyo Mfilisti katika hema lake mwenyewe. \p \v 55 Sauli alipomwona Daudi anaenda kukabiliana na huyo Mfilisti, alimwambia Abneri, jemadari wa jeshi, “Abneri, yule kijana ni mwana wa nani?” \p Abneri akajibu, “Hakika kama uishivyo, ee mfalme, mimi sifahamu.” \p \v 56 Mfalme akasema, “Uliza huyu kijana ni mwana wa nani.” \p \v 57 Mara Daudi aliporudi kutoka kumuua huyo Mfilisti, Abneri akamchukua na kumleta mbele ya Sauli. Daudi alikuwa bado anakishikilia kichwa cha yule Mfilisti. \p \v 58 Sauli akamuuliza, “Kijana, wewe ni mwana wa nani?” \p Daudi akasema, “Mimi ni mwana wa mtumishi wako Yese wa Bethlehemu.” \c 18 \s1 Sauli amwonea Daudi wivu \p \v 1 Baada ya Daudi kumaliza kuongea na Sauli, roho ya Yonathani ikaambatana na roho ya Daudi, naye akampenda kama nafsi yake mwenyewe. \v 2 Kuanzia siku ile Sauli akamchukua Daudi naye hakumruhusu kurudi nyumbani mwa baba yake. \v 3 Yonathani akafanya agano na Daudi kwa sababu alimpenda kama nafsi yake mwenyewe. \v 4 Yonathani akavua joho alilokuwa amevaa na kumpa Daudi, pamoja na koti lake, silaha zake, hata pamoja na upanga wake, upinde wake na mshipi wake. \p \v 5 Lolote Sauli alilomtuma Daudi kufanya, alifanikiwa sana, hata Sauli akampa cheo cha juu katika jeshi. Jambo hili likawapendeza watu wote, hata maafisa wa Sauli pia. \p \v 6 Watu walipokuwa wanarudi nyumbani baada ya Daudi kumuua yule Mfilisti, wanawake wakaja kutoka pande zote za miji ya Israeli kumlaki Mfalme Sauli kwa kuimba na kucheza, kwa nyimbo za furaha na kwa matari na zeze. \p \v 7 Walipokuwa wanacheza, wakaimba: \q1 “Sauli amewaua elfu zake, \q2 naye Daudi makumi elfu yake.” \p \v 8 Sauli akakasirika sana; sehemu hii ya kurudia rudia ya wimbo huu ilimkasirisha sana. Akafikiri kuwa, “Wamempa Daudi makumi elfu, lakini mimi wamenipa elfu tu. Apate nini zaidi isipokuwa ufalme?” \v 9 Kuanzia wakati ule na kuendelea Sauli akawa na jicho la wivu juu ya Daudi. \p \v 10 Kesho yake roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikaja kwa nguvu juu ya Sauli. Alikuwa akitabiri nyumbani mwake, wakati Daudi alikuwa akipiga kinubi, kama alivyozoea. Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake; \v 11 akautupa kwa nguvu, akijiambia mwenyewe, “Nitamchoma kwa mkuki abaki hapo ukutani.” Lakini Daudi akamkwepa mara mbili. \p \v 12 Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Daudi, lakini alikuwa amemwacha yeye. \v 13 Kwa hiyo Sauli akamwondoa Daudi mbele yake na kumpa kuwa kiongozi wa watu elfu moja, naye Daudi akatoka na kuingia akiongoza vikosi katika vita. \v 14 Katika kila kitu alichofanya, Daudi alipata mafanikio makubwa, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja naye. \v 15 Sauli alipoona jinsi alivyokuwa akifanikiwa, akamwogopa. \v 16 Lakini Israeli wote na Yuda walimpenda Daudi, kwa sababu ndiye alikuwa akiwaongoza katika vita vyao. \p \v 17 Sauli akamwambia Daudi, “Huyu hapa binti yangu mkubwa Merabu. Nitakupa umwoe, endapo tu utanitumikia kwa ushujaa na kupigana vita vya Mwenyezi Mungu.” Kwa maana Sauli alisema moyoni mwake, “Sitainua mkono wangu dhidi yake. Acha mkono wa Wafilisti uwe juu yake.” \p \v 18 Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mimi ni nani, nayo jamaa yangu ni nini au ukoo wa baba yangu katika Israeli, kwamba mimi niwe mkwewe mfalme?” \v 19 Basi ulipofika wakati wa Daudi kupewa Merabu, binti Sauli, huyo binti aliozwa kwa Adrieli, Mmeholathi. \p \v 20 Basi Mikali binti Sauli alimpenda Daudi, nao walipomwambia Sauli kuhusu jambo hili, likampendeza. \v 21 Sauli akawaza, “Nitampa Daudi binti yangu, ili apate kuwa mtego kwake, ili mkono wa Wafilisti upate kuwa juu yake.” Hivyo Sauli akamwambia Daudi, “Sasa unayo nafasi ya pili ya kuwa mkwe wangu.” \p \v 22 Ndipo Sauli akawaagiza watumishi wake, akisema, “Zungumzeni na Daudi kwa siri na kumwambia, ‘Tazama, mfalme amependezwa nawe, nao watumishi wake wote wanakupenda. Basi na uwe mkwewe mfalme.’ ” \p \v 23 Watumishi wa Sauli wakarudia hayo maneno kwa Daudi. Lakini Daudi akasema, “Je, mnafikiri ni jambo dogo kuwa mkwewe mfalme? Mimi ni mtu maskini tu, na nisiyejulikana sana.” \p \v 24 Watumishi wa Sauli walipomweleza vile Daudi alivyosema, \v 25 Sauli akajibu, “Mwambieni Daudi, ‘Mfalme hataki zawadi nyingine kuwa mahari, isipokuwa magovi mia moja ya Wafilisti, ili kulipiza kisasi juu ya adui zake.’ ” Mawazo ya Sauli yalikuwa Daudi akaanguke mikononi mwa Wafilisti. \p \v 26 Watumishi walipomwambia Daudi mambo haya, ikampendeza kuwa mkwewe mfalme. Basi kabla siku iliyopangwa haijafika, \v 27 Daudi na watu wake walitoka na kuwaua Wafilisti mia mbili. Akayaleta magovi yao na kupeleka hesabu kamilifu kwa mfalme, ili apate kuwa mkwewe mfalme. Ndipo Sauli akamwoza Daudi Mikali binti yake. \p \v 28 Sauli alipotambua kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Daudi na kwamba Mikali binti yake anampenda Daudi, \v 29 Sauli akazidi kumwogopa Daudi, naye Sauli akabaki kuwa adui yake siku zote za maisha yake. \p \v 30 Majemadari wa jeshi la Wafilisti waliendelea kupigana vita na kadiri walivyoendelea kupigana, Daudi akazidi kutenda kwa hekima kuliko maafisa wengine wa Sauli, nalo jina lake likajulikana sana. \c 19 \s1 Sauli ajaribu kumuua Daudi \p \v 1 Sauli akamwambia mwanawe Yonathani na watumishi wake wote wamuue Daudi. Lakini Yonathani mwana wa Sauli alimpenda sana Daudi. \v 2 Yonathani akamwonya Daudi, akisema, “Baba yangu Sauli anatafuta nafasi ya kukuua. Ujilinde kesho asubuhi, nenda mahali pa siri na ukae huko. \v 3 Nitatoka na kukaa na baba yangu shambani mahali uliko. Nitazungumza naye juu yako, nami nitakueleza nitakachogundua.” \p \v 4 Yonathani akanena mema kuhusu Daudi kwa Sauli baba yake na kumwambia, “Mfalme asitende mabaya kwa mtumishi wake Daudi; hajakukosea, aliyoyafanya yamekuwa ya faida sana kwako. \v 5 Alihatarisha maisha yake alipomuua yule Mfilisti. Mwenyezi Mungu akajipatia ushindi mkubwa kwa ajili ya Israeli wote, nawe uliuona na ukafurahi. Kwa nini basi utende mabaya kwa mtu asiye na hatia kama Daudi kwa kumuua bila sababu?” \p \v 6 Sauli akamsikiliza Yonathani na kuapa hivi: “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, Daudi hatauawa.” \p \v 7 Basi Yonathani akamwita Daudi na kumweleza mazungumzo yote. Akamleta kwa Sauli, naye Daudi akawa pamoja na Sauli kama kwanza. \p \v 8 Vita vilitokea tena, naye Daudi akatoka na kupigana na Wafilisti. Akawapiga kwa nguvu nyingi hata wakakimbia mbele yake. \p \v 9 Lakini roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mwenyezi Mungu ikaja juu ya Sauli alipokuwa ameketi katika nyumba yake akiwa na mkuki mkononi mwake. Daudi alipokuwa anampigia kinubi, \v 10 Sauli akajaribu kumchomea Daudi ukutani kwa huo mkuki wake, lakini Daudi akauhepa huo mkuki wa Sauli ukakita ukutani. Usiku ule ule Daudi akakimbia na kuokoka. \p \v 11 Sauli akatuma watu nyumbani mwa Daudi wailinde hiyo nyumba na kumuua asubuhi. Lakini Mikali, mkewe Daudi, akamwonya akisema, “Usipokimbia kuokoa maisha yako usiku huu, kesho utauawa.” \v 12 Basi Mikali akamteremsha Daudi kupitia dirishani, naye akakimbia na kuokoka. \v 13 Kisha Mikali akachukua kinyago, akakilaza kitandani, akakifunika kwa vazi na kukiwekea singa za mbuzi kichwani. \p \v 14 Sauli alipotuma watu kumkamata Daudi, Mikali akasema, “Yeye ni mgonjwa.” \p \v 15 Kisha Sauli akatuma watu tena kumwona Daudi naye akawaambia, “Mleteni kwangu juu ya kitanda chake ili nipate kumuua.” \v 16 Lakini wale watu walipoingia, kumbe ni kinyago tu kilichokuwa kitandani, na kwenye kichwa kulikuwa na singa za mbuzi. \p \v 17 Sauli akamwambia Mikali, “Kwa nini umenidanganya mimi hivi na kumwacha adui yangu aende zake ili apate kuokoka?” \p Mikali akamwambia, “Yeye aliniambia, ‘Niache niende zangu. Kwa nini nikuue?’ ” \p \v 18 Daudi alipokuwa amekimbia na kuokoka, alimwendea Samweli huko Rama na kumwambia yale yote Sauli alimfanyia. Ndipo Daudi na Samweli wakaenda Nayothi kukaa huko. \v 19 Habari zikamfikia Sauli kusema: “Daudi yuko Nayothi huko Rama.” \v 20 Basi Sauli akatuma watu kumkamata Daudi, lakini walipoona kundi la manabii wakitoa unabii, wakiwa pamoja na Samweli akiwa amesimama hapo kama kiongozi wao, Roho wa Mungu akaja juu ya watu wa Sauli, nao pia wakatoa unabii. \v 21 Sauli akaelezwa hilo, naye akapeleka watu wengine zaidi, nao wakatoa unabii pia. Sauli akatuma watu mara ya tatu, nao pia wakatoa unabii. \v 22 Mwishowe, yeye mwenyewe akaondoka kwenda Rama na kwenda hadi kwenye kile kisima kikubwa kilichoko huko Seku. Naye akauliza, “Wako wapi Samweli na Daudi?” \p Wakasema, “Wako Nayothi huko Rama.” \p \v 23 Hivyo Sauli akaenda Nayothi huko Rama. Lakini Roho wa Mungu akaja juu yake hata yeye, akawa anatembea huku anatoa unabii hadi akafika Nayothi. \v 24 Akavua majoho yake na pia akatoa unabii mbele ya Samweli. Akalala hali hiyo ule mchana kutwa na usiku kucha. Hii ndiyo sababu watu husema, “Je, Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?” \c 20 \s1 Daudi na Yonathani \p \v 1 Kisha Daudi akakimbia kutoka Nayothi huko Rama akamwendea Yonathani na kumuuliza, “Kwani nimefanya nini? Kosa langu ni nini? Nimemkosea baba yako kwa jinsi gani, hata kwamba anajaribu kuniua?” \p \v 2 Yonathani akajibu, “La hasha! Hutakufa! Tazama, baba yangu hafanyi kitu chochote, kikubwa au kidogo, bila kuniambia mimi. Kwa nini anifiche hili? Sivyo ilivyo!” \p \v 3 Lakini Daudi akaapa na kusema, “Baba yako anajua kabisa kwamba nimepata kibali mbele yako, naye amesema moyoni mwake, ‘Yonathani sharti asilijue hili, la sivyo atahuzunika.’ Lakini hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na kama uishivyo, kuna hatua moja tu kati yangu na mauti.” \p \v 4 Yonathani akamwambia Daudi, “Chochote unachotaka nifanye, nitakufanyia.” \p \v 5 Basi Daudi akamwambia Yonathani, “Angalia, kesho ni sikukuu ya Mwezi Mwandamo, nami inanipasa kula chakula pamoja na mfalme; lakini niache niende kujificha shambani hadi kesho kutwa. \v 6 Kama baba yako akiona ya kuwa sipo, mwambie, ‘Daudi aliniomba sana ruhusa kuwahi Bethlehemu, mji wake wa nyumbani, kwa sababu dhabihu ya mwaka inafanywa huko kwa ajili ya ukoo wake wote.’ \v 7 Akisema, ‘Ni vyema sana,’ basi mtumishi wako yu salama. Lakini akikasirika, unaweza kuwa na hakika kwamba anakusudia kunidhuru. \v 8 Kwako wewe, mtende wema mtumishi wako, kwa sababu mmeingia kwenye agano naye mbele za Mwenyezi Mungu. Nikiwa na hatia, basi niue wewe mwenyewe! Kwa nini unikabidhi kwa baba yako?” \p \v 9 Yonathani akasema, “La hasha! Kama ningekuwa na kidokezo kidogo kwamba baba yangu amekusudia kukudhuru wewe, je, nisingekuambia?” \p \v 10 Daudi akamuuliza Yonathani, “Je, nani atakayeniambia kama baba yako atakujibu kwa ukali?” \p \v 11 Yonathani akamwambia, “Njoo, twende shambani.” Basi wakaenda huko pamoja. \p \v 12 Kisha Yonathani akamwambia Daudi, “Ninakuahidi kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, hakika nitamchunguza baba yangu wakati kama huu kesho kutwa! Kama ameweka utaratibu wa kufaa kukuhusu wewe, je, sitakutumia ujumbe na kukufahamisha? \v 13 Lakini ikiwa baba yangu amenuia kukudhuru, Mwenyezi Mungu na aniadhibu vikali zaidi iwapo sitakufahamisha na kukuaga uende salama. Mwenyezi Mungu na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na baba yangu. \v 14 Lakini nitendee wema usiokoma kama ule wa Mwenyezi Mungu siku zote za maisha yangu, ili nisije nikauawa, \v 15 wala usiuondoe wema wako kwa jamaa yangu, hata kama ni wakati ule Mwenyezi Mungu atakapokuwa amekatilia mbali kila adui wa Daudi kutoka uso wa dunia.” \p \v 16 Basi Yonathani akafanya agano na nyumba ya Daudi, akisema: “Mwenyezi Mungu na awaangamize adui za Daudi.” \v 17 Naye Yonathani akamtaka Daudi athibitishe tena kiapo chake cha kumpenda, kwa sababu Yonathani alimpenda Daudi kama nafsi yake mwenyewe. \p \v 18 Kisha Yonathani akamwambia Daudi, “Kesho ni sikukuu ya Mwezi Mwandamo. Itajulikana kwamba haupo kwa kuwa kiti chako kitakuwa wazi. \v 19 Kesho kutwa, inapokaribia jioni, nenda mahali pale ulipojificha wakati tatizo hili lilipoanza na usubiri karibu na jiwe la Ezeli. \v 20 Nitapiga mishale mitatu kando yake, kana kwamba nilienda kulenga shabaha. \v 21 Kisha nitamtuma mvulana na kumwambia, ‘Nenda ukaitafute mishale.’ Nikimwambia, ‘Tazama mishale iko upande huu wako! Uilete hapa,’ basi uje, kwa sababu hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, wewe ni salama, hakuna hatari. \v 22 Lakini nikimwambia huyo mvulana, ‘Angalia, mishale iko mbele yako,’ basi inakupasa uondoke, kwa sababu Mwenyezi Mungu amekuruhusu uende zako. \v 23 Kuhusu yale tuliyozungumza wewe na mimi: kumbuka, Mwenyezi Mungu ndiye shahidi kati yako wewe na mimi milele.” \p \v 24 Basi Daudi akajificha shambani, na sikukuu ya Mwezi Mwandamo ilipowadia, mfalme akaketi ili ale. \v 25 Akaketi mahali pake pa kawaida karibu na ukuta, kuelekeana na Yonathani, naye Abneri akaketi karibu na Mfalme Sauli, lakini kiti cha Daudi kilikuwa wazi. \v 26 Sauli hakusema chochote siku ile kwa kuwa alifikiri, “Kuna kitu cha lazima kimetokea kwa Daudi ambacho kimemfanya najisi asihudhurie karamu; hakika yeye yu najisi.” \v 27 Lakini siku iliyofuata, siku ya pili ya mwezi, kiti cha Daudi kilikuwa wazi tena. Kisha Sauli akamwambia mwanawe Yonathani, “Kwa nini mwana wa Yese hajaja chakulani jana wala leo?” \p \v 28 Yonathani akamjibu, “Daudi alinisihi sana nimpe ruhusa aende Bethlehemu. \v 29 Alisema, ‘Niruhusu niende, kwa sababu jamaa yetu wana dhabihu mjini, na ndugu yangu ameniagiza niwepo huko. Kama nimepata kibali mbele yako, niruhusu niende kuona ndugu zangu.’ Hii ndiyo sababu hakuja mezani pa mfalme.” \p \v 30 Hasira ya Sauli ikawaka dhidi ya Yonathani na kumwambia, “Wewe mwana wa mwanamke mkaidi na mwasi! Je, sijui kuwa umekuwa upande wa mwana wa Yese kwa aibu yako mwenyewe na kwa aibu ya mama yako aliyekuzaa? \v 31 Maadamu mwana wa Yese angali anaishi katika dunia hii wewe wala ufalme wako hautasimama. Sasa tuma aitwe umlete kwangu, kwa kuwa ni lazima afe!” \p \v 32 Yonathani akamuuliza baba yake, “Kwa nini auawe? Kwani amefanya nini?” \v 33 Lakini Sauli akamtupia Yonathani mkuki wake kwa nguvu ili amuue. Hapo ndipo Yonathani alipotambua kwamba baba yake alikusudia kumuua Daudi. \p \v 34 Yonathani akainuka kutoka mezani kwa hasira kali. Siku ile ya pili ya mwezi hakula chakula, kwa kuwa alikuwa amehuzunishwa na vitendo vya aibu ambavyo baba yake alikuwa anamtendea Daudi. \p \v 35 Kesho yake asubuhi Yonathani alienda shambani kukutana na Daudi. Alikuwa amefuatana na mvulana mdogo, \v 36 naye Yonathani akamwambia yule mvulana, “Kimbia ukatafute mishale nitakayorusha.” Mvulana alipokuwa akikimbia, akarusha mishale mbele yake. \v 37 Yule mvulana alipofika mahali pale mshale wa Yonathani ulikuwa umeanguka, Yonathani akamwita, “Je, mshale hauko mbele yako?” \v 38 Yonathani akampigia kelele, “Harakisha, nenda haraka! Usisimame!” Mvulana akaokota mshale na kurudi kwa bwana wake. \v 39 (Mvulana hakujua chochote kuhusu hayo yote; Yonathani na Daudi tu ndio waliojua.) \v 40 Basi Yonathani akampa yule mvulana silaha zake na kumwambia, “Nenda, zirudishe mjini.” \p \v 41 Baada ya mvulana kwenda, Daudi akainuka kutoka upande wa kusini wa lile jiwe, naye akasujudu mara tatu mbele ya Yonathani. Kisha kila mmoja akambusu mwenzake, wakalia pamoja. Lakini Daudi akalia zaidi. \p \v 42 Yonathani akamwambia Daudi, “Nenda kwa amani, kwa kuwa tumeapiana kiapo cha urafiki kati yetu kwa jina la Mwenyezi Mungu, tukisema, ‘Mwenyezi Mungu ndiye shahidi kati yako na mimi, na kati ya wazao wako na wazao wangu milele.’ ” Kisha Daudi akaondoka, naye Yonathani akarudi mjini. \c 21 \s1 Daudi huko Nobu \p \v 1 Daudi akaenda Nobu, kwa Ahimeleki kuhani. Ahimeleki akatetemeka alipokutana naye, akamuuliza, “Kwa nini uko peke yako? Kwa nini hukufuatana na mtu yeyote?” \p \v 2 Daudi akamjibu Ahimeleki kuhani, akisema, “Mfalme ameniagiza shughuli fulani na kuniambia, ‘Mtu yeyote asijue chochote kuhusu kazi niliyokutuma kuifanya, wala maagizo niliyokupa!’ Kuhusu watu wangu, nimewaambia mahali pa kukutana. \v 3 Sasa basi, una nini mkononi? Nipatie mikate mitano au chochote unachoweza kupata.” \p \v 4 Lakini kuhani akamjibu Daudi, “Sina mkate wowote wa kawaida kwa sasa. Hata hivyo, ipo hapa mikate iliyowekwa wakfu, iwapo watu wamejitenga na wanawake.” \p \v 5 Daudi akajibu, “Hakika tumejitenga na wanawake kwa siku hizi chache kama kawaida ya ninapotoka kwenda kwenye shughuli. Navyo vyombo vya wale vijana huwa ni vitakatifu hata kwenye safari ya kawaida, si zaidi sana leo vyombo vyao vitakuwa ni vitakatifu?” \v 6 Hivyo kuhani akampa ile mikate iliyowekwa wakfu, kwa kuwa hapakuwa na mikate mingine isipokuwa hiyo ya Wonesho, iliyokuwa imeondolewa hapo mbele za Mwenyezi Mungu na kubadilishwa na mingine yenye moto siku ile ilipoondolewa. \p \v 7 Basi siku hiyo palikuwepo mmoja wa watumishi wa Sauli, aliyezuiliwa mbele za Mwenyezi Mungu; alikuwa Doegi Mwedomu, kiongozi wa wachungaji wa Sauli. \p \v 8 Daudi akamuuliza Ahimeleki, “Je, unao mkuki au upanga hapa? Sikuleta upanga wala silaha nyingine yoyote, kwa sababu shughuli ya mfalme ilikuwa ya haraka.” \p \v 9 Kuhani akajibu, “Upanga wa Goliathi Mfilisti, ambaye ulimuua katika Bonde la Ela, upo hapa, umefungwa katika kitambaa nyuma ya kizibau. Kama unauhitaji, uchukue, hakuna upanga mwingine hapa ila huo tu.” \p Daudi akasema, “Hakuna upanga mwingine kama huo. Nipatie huo.” \s1 Daudi huko Gathi \p \v 10 Siku ile Daudi akamkimbia Sauli na kwenda kwa Akishi mfalme wa Gathi. \v 11 Nao watumishi wa Akishi wakamwambia, “Je, huyu si ndiye Daudi mfalme wa nchi? Je, huyu si ndiye yule ambaye wanaimba katika ngoma zao wakisema: \q1 “ ‘Sauli amewaua elfu zake, \q2 naye Daudi makumi elfu yake’?” \p \v 12 Daudi akayaweka maneno haya moyoni naye akamwogopa sana Akishi mfalme wa Gathi. \v 13 Basi akajifanya mwendawazimu mbele yao; naye alipokuwa mikononi mwao, alitenda kama kichaa, akikwaruza kwa kutia alama juu ya milango ya lango, na kuachia mate kutiririka kwenye ndevu zake. \p \v 14 Akishi akawaambia watumishi wake, “Tazameni mtu huyu! Ana wazimu! Kwa nini mnamleta kwangu? \v 15 Je, mimi nimepungukiwa na wenda wazimu kiasi kwamba mmeniletea mtu huyo hapa aendelee kufanya hivi mbele yangu? Je, ilikuwa ni lazima mtu huyo aje nyumbani mwangu?” \c 22 \s1 Daudi akiwa Adulamu na Mispa \p \v 1 Daudi akaondoka Gathi na kukimbilia kwenye pango la Adulamu. Ndugu zake na watu wa nyumba ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. \v 2 Wale wote waliokuwa katika dhiki au waliokuwa na madeni au wale ambao hawakuridhika wakamkusanyikia Daudi, naye akawa kiongozi wao. Watu wapatao mia nne walikuwa naye. \p \v 3 Kutoka huko Daudi akaenda Mispa iliyoko Moabu na kumwambia mfalme wa Moabu, “Naomba uwaruhusu baba yangu na mama yangu waje kukaa nawe hadi nijue nini Mungu atakachonifanyia.” \v 4 Hivyo akawaacha wazazi wake wakae na mfalme wa Moabu, nao wakakaa naye muda wote ambao Daudi alikuwa ngomeni. \p \v 5 Ndipo nabii Gadi akamwambia Daudi, “Usikae ngomeni. Nenda katika nchi ya Yuda.” Hivyo Daudi akaondoka na kwenda katika msitu wa Herethi. \s1 Sauli awaua makuhani wa Nobu \p \v 6 Basi Sauli akasikia kwamba Daudi na watu wake wameonekana. Sauli akiwa na mkuki mkononi, alikuwa ameketi chini ya mti wa mkwaju kwenye kilima huko Gibea, maafisa wake wote wakiwa wamesimama kumzunguka. \v 7 Sauli akawaambia, “Sikilizeni enyi Wabenyamini! Je, mwana wa Yese atawapa ninyi nyote mashamba na mashamba ya mizabibu? Je, atawafanya ninyi nyote majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia? \v 8 Je, ndiyo sababu ninyi mkapanga hila mbaya dhidi yangu? Hakuna hata mmoja wenu ambaye ameniambia ni lini mwanangu alifanya agano na mwana wa Yese. Hapana hata mmoja wenu anayejishughulisha nami wala anayeniambia kwamba mwanangu amechochea mtumishi wangu kunivizia, kama afanyavyo leo.” \p \v 9 Lakini Doegi Mwedomu, aliyekuwa akisimama na maafisa wa Sauli, akasema, “Nilimwona mwana wa Yese akija kwa Ahimeleki mwana wa Ahitubu huko Nobu. \v 10 Ahimeleki akamuuliza Mwenyezi Mungu kwa ajili yake; pia akampa vyakula na ule upanga wa Goliathi Mfilisti.” \p \v 11 Kisha mfalme akatuma watu wamwite kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, waliokuwa makuhani huko Nobu, nao wote wakaja kwa mfalme. \v 12 Sauli akasema, “Sikiliza sasa, mwana wa Ahitubu.” \p Akajibu, “Naam, bwana wangu.” \p \v 13 Sauli akamwambia, “Kwa nini umepanga njama dhidi yangu, wewe na mwana wa Yese, ukampa vyakula na upanga, tena, ulimuuliza Mungu kwa ajili yake na kwa sababu hiyo ameasi dhidi yangu na kunivizia, kama afanyavyo leo?” \p \v 14 Ahimeleki akamjibu mfalme, “Ni nani miongoni mwa watumishi wako wote aliye mwaminifu kama Daudi, mkwewe mfalme, kiongozi wa walinzi wako na anayeheshimika sana katika watu wa nyumbani mwako? \v 15 Je, siku hiyo ilikuwa ndiyo ya kwanza kumwomba Mungu kwa ajili yake? La hasha! Mfalme na usiwashutumu watumishi wako wala yeyote wa jamaa ya baba yake, kwa kuwa mtumishi wako hafahamu lolote kabisa kuhusu jambo hili lote.” \p \v 16 Lakini mfalme akasema, “Ahimeleki, hakika utakufa, wewe na jamaa yote ya baba yako.” \p \v 17 Ndipo mfalme akawaamuru walinzi wake waliokuwa kando yake: “Geukeni na kuwaua makuhani wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu nao pia wamejiunga na Daudi. Walijua kuwa alikuwa anakimbia, wala hawakuniambia.” \p Lakini maafisa wa mfalme hawakuwa radhi kuinua mkono kuwaua makuhani wa Mwenyezi Mungu. \p \v 18 Kisha mfalme akamwagiza Doegi, “Wewe geuka ukawaue makuhani.” Hivyo basi Doegi Mwedomu, akageuka na kuwaua. Siku ile aliwaua watu themanini na watano waliovaa vizibau vya kitani. \v 19 Pia akaupiga Nobu, mji wa makuhani kwa upanga, wakiwemo wanaume na wanawake, watoto na wale watoto wanaonyonya, ng’ombe, punda na kondoo wake. \p \v 20 Lakini Abiathari, mwana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akatoroka, akakimbia na kujiunga na Daudi. \v 21 Abiathari akamwambia Daudi kuwa Sauli amewaua makuhani wa Mwenyezi Mungu. \v 22 Kisha Daudi akamwambia Abiathari: “Siku ile Doegi Mwedomu alipokuwa pale, nilijua atahakikisha amemwambia Sauli kuwa mimi ninawajibika kwa vifo vya jamaa yote ya baba yako. \v 23 Kaa pamoja nami; usiogope. Mtu anayeutafuta uhai wako anautafuta uhai wangu pia. Ukiwa pamoja nami utakuwa salama.” \c 23 \s1 Daudi aokoa Keila \p \v 1 Daudi alipoambiwa, “Tazama, Wafilisti wanapigana dhidi ya Keila, nao wanapokonya nafaka katika sakafu za kupuria,” \v 2 akauliza kwa Mwenyezi Mungu, akisema, “Je, niende na kuwashambulia hawa Wafilisti?” \p Mwenyezi Mungu akamjibu, “Nenda, washambulie Wafilisti na uuokoe Keila.” \p \v 3 Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Hapa Yuda kwenyewe tunaogopa. Je, si zaidi tukienda Keila dhidi ya majeshi ya Wafilisti!” \p \v 4 Daudi akauliza kwa Mwenyezi Mungu tena, naye Mwenyezi Mungu akamjibu akamwambia, “Shuka uende Keila, kwa kuwa nitawatia Wafilisti mkononi mwako.” \v 5 Basi Daudi na watu wake wakaenda Keila, wakapigana na Wafilisti na kutwaa wanyama wao wa kutosha. Daudi akawatia hasara kubwa Wafilisti na kuwaokoa watu wa Keila. \v 6 Basi Abiathari mwana wa Ahimeleki alikuwa ameleta kizibau alipokimbilia kwa Daudi huko Keila. \s1 Sauli amfuata Daudi \p \v 7 Sauli akaambiwa kwamba Daudi alikuwa ameenda Keila, naye akasema, “Mungu amemtia mkononi mwangu, kwa kuwa Daudi amejifunga mwenyewe kwa kuingia kwenye mji wenye malango na makomeo.” \v 8 Naye Sauli akayaita majeshi yake yote yaende vitani, kuishukia Keila ili kumzingira Daudi na watu wake kwa jeshi. \p \v 9 Daudi alipojua kuwa Sauli alikuwa ana hila dhidi yake, akamwambia Abiathari kuhani, “Leta kile kizibau.” \v 10 Daudi akasema, “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mtumishi wako amesikia kwa hakika kwamba Sauli anapanga kuja Keila na kuangamiza mji kwa ajili yangu. \v 11 Je, watu wa Keila watanisalimisha kwake? Je, Sauli atateremka, kama mtumishi wako alivyosikia? Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mwambie mtumishi wako.” \p Naye Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, atashuka.” \p \v 12 Daudi akauliza tena, “Je watu wa Keila watanisalimisha mimi pamoja na watu wangu kwa Sauli?” \p Naye Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, watafanya hivyo.” \p \v 13 Basi Daudi na watu wake wapatao mia sita wakaondoka Keila, wakawa wanaenda sehemu moja hadi nyingine. Sauli alipoambiwa Daudi ametoroka kutoka Keila, hakuenda huko. \p \v 14 Daudi akakaa katika ngome za jangwani na katika vilima vya Jangwa la Zifu. Siku baada ya siku Sauli aliendelea kumsaka, lakini Mungu hakumtia Daudi mkononi mwake. \p \v 15 Daudi alipokuwa huko Horeshi katika Jangwa la Zifu, akajua kuwa Sauli alikuwa amekuja ili amuue. \v 16 Naye Yonathani mwana wa Sauli akamwendea Daudi huko Horeshi na kumtia moyo kusimama imara katika imani yake kwa Mungu. \v 17 Akamwambia, “Usiogope, Daudi; baba yangu Sauli hatakutia mkononi mwake. Utakuwa mfalme juu ya Israeli, nami nitakuwa wa pili wako. Hata baba yangu Sauli anajua hili.” \v 18 Wote wawili wakafanya agano mbele za Mwenyezi Mungu. Kisha Yonathani akaenda zake nyumbani, lakini Daudi akabaki Horeshi. \p \v 19 Basi Wazifu wakakwea kwa Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hajifichi miongoni mwetu katika ngome huko Horeshi, katika kilima cha Hakila, kusini mwa Yeshimoni? \v 20 Sasa, ee mfalme, uteremke wakati wowote unapoona vyema kufanya hivyo, sisi tutawajibika kumkabidhi kwa mfalme.” \p \v 21 Sauli akajibu, “Mwenyezi Mungu awabariki kwa kunifikiria. \v 22 Nendeni mkafanye maandalizi zaidi. Mkajue mahali Daudi huenda mara kwa mara, na nani amepata kumwona huko. Wananiambia yeye ni mjanja sana. \v 23 Jueni kila mahali anapojificha, kisha mrudi na kunipa taarifa kamili. Nami nitaenda pamoja nanyi; kama atakuwa katika eneo hilo, nitamsaka miongoni mwa koo zote za Yuda.” \p \v 24 Basi wakaondoka na kwenda hadi Zifu wakimtangulia Sauli. Naye Daudi na watu wake walikuwa katika Jangwa la Maoni, katika Araba kusini mwa Yeshimoni. \v 25 Sauli na watu wake wakaanza msako, naye Daudi alipoelezwa hili, akateremka hadi mwambani na kukaa katika Jangwa la Maoni. Sauli aliposikia hili, akaenda katika Jangwa la Maoni akimfuata Daudi. \p \v 26 Sauli alikuwa akienda upande mmoja wa mlima, naye Daudi na watu wake walikuwa upande mwingine wa mlima, wakiharakisha kumkimbia Sauli. Sauli na majeshi yake walipokaribia kumkamata Daudi na watu wake, \v 27 mjumbe alikuja kwa Sauli, akisema, “Njoo haraka! Wafilisti wanaishambulia nchi.” \v 28 Ndipo Sauli akarudi akaacha kumfuata Daudi na kwenda kukabiliana na Wafilisti. Ndiyo sababu wanaiita sehemu hii Sela-Hamalekothi\f + \fr 23:28 \fr*\ft maana yake \ft*\fqa Mwamba wa Kutengana\fqa*\f*. \v 29 Naye Daudi akakwea kutoka huko na kuishi katika ngome za En-Gedi. \c 24 \s1 Daudi amwacha Sauli hai \p \v 1 Baada ya Sauli kurudi kuwafuatia Wafilisti, akaambiwa kwamba, “Daudi yuko katika Jangwa la En-Gedi.” \v 2 Basi Sauli akachukua vijana wenye uwezo elfu tatu kutoka Israeli yote kwenda kumtafuta Daudi na watu wake karibu na Majabali ya Mbuzi-Mwitu. \p \v 3 Akaja kwenye mazizi ya kondoo kando ya njia, hapo palikuwa na pango, na Sauli akaingia ndani kujipumzisha. Daudi na watu wake walikuwa wamo mle pangoni kwa ndani zaidi. \v 4 Watu wa Daudi wakasema, “Hii ndiyo siku aliyonena Mwenyezi Mungu akikuambia, ‘Nitamtia adui yako mikononi mwako ili wewe umtendee utakavyo.’ ” Basi Daudi akanyemelea bila kuonekana na kukata upindo wa joho la Sauli. \p \v 5 Baada ya hilo, dhamiri ya Daudi ikataabika kwa kukata upindo wa joho la Sauli. \v 6 Akawaambia watu wake, “Mwenyezi Mungu na apishie mbali nisije nikafanya jambo kama hilo kwa bwana wangu, yeye ambaye ni mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu, au kuinua mkono wangu dhidi yake; kwani yeye ni mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu.” \v 7 Kwa maneno haya Daudi akawaonya watu wake na hakuwaruhusu wamshambulie Sauli. Naye Sauli akaondoka pangoni na kwenda zake. \p \v 8 Ndipo Daudi naye akatoka pangoni na kumwita Sauli akisema, “Mfalme, bwana wangu!” Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama na kumsujudia, uso wake ukigusa chini. \v 9 Akamwambia Sauli, “Kwa nini unasikiliza wakati watu wanapokuambia, ‘Daudi amenuia kukudhuru’? \v 10 Leo umeona kwa macho yako mwenyewe jinsi Mwenyezi Mungu alivyokutia mikononi mwangu huko pangoni. Watu wengine walisisitiza nikuue, lakini nilikuacha, nikisema, ‘Sitainua mkono wangu dhidi ya bwana wangu, kwa sababu yeye ni mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu.’ \v 11 Tazama, baba yangu, ona kipande hiki cha joho lako mkononi mwangu! Nilikata upindo wa joho lako lakini sikukuua. Basi ujue na kutambua kuwa sina hatia ya kutenda mabaya wala kuasi. Wewe sijakukosea, lakini wewe unaniwinda mimi ili kuniua. \v 12 Mwenyezi Mungu na ahukumu kati yangu na wewe. Naye Mwenyezi Mungu alipize mabaya unayonitendea, lakini mkono wangu hautakugusa. \v 13 Kama msemo wa kale usemavyo, ‘Kutoka kwa watenda maovu hutoka matendo maovu,’ kwa hiyo mkono wangu hautakugusa wewe. \p \v 14 “Je, mfalme wa Israeli ametoka dhidi ya nani? Ni nani unayemfuatia? Je, ni mbwa mfu? Ni kiroboto? \v 15 Mwenyezi Mungu na awe mwamuzi wetu, yeye na aamue kati yetu. Yeye na anitetee shauri langu; anihesabie haki kwa kuniokoa mkononi mwako.” \p \v 16 Daudi alipomaliza kusema haya, Sauli akamuuliza, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Ndipo Sauli akalia kwa sauti kuu. \v 17 Akamwambia Daudi, “Wewe ni mwenye haki kuliko mimi; umenitendea mema, lakini mimi nimekutendea mabaya. \v 18 Sasa umeniambia kuhusu mema uliyonitendea. Mwenyezi Mungu alinitia mikononi mwako, lakini wewe hukuniua. \v 19 Je, mtu ampatapo adui yake, humwacha aende zake bila kumdhuru? Mwenyezi Mungu na akulipe mema kwa jinsi ulivyonitenda leo. \v 20 Ninajua kwamba hakika utakuwa mfalme na kwamba ufalme wa Israeli utakuwa imara mikononi mwako. \v 21 Sasa niapie kwa Mwenyezi Mungu kwamba hutakatilia mbali uzao wangu wala kulifuta jina langu kutoka jamaa ya baba yangu.” \p \v 22 Basi Daudi akamwapia Sauli. Kisha Sauli akarudi zake nyumbani, lakini Daudi na watu wake wakapanda kwenda ngomeni. \c 25 \s1 Daudi, Nabali na Abigaili \p \v 1 Basi Samweli akafa, nao Waisraeli wote wakakusanyika na kumwombolezea; wakamzika nyumbani mwake huko Rama. \p Kisha Daudi akateremka kwenye Jangwa la Parani. \v 2 Mtu mmoja huko Maoni, aliyekuwa na makao huko Karmeli, alikuwa tajiri sana. Alikuwa na mbuzi elfu moja na kondoo elfu tatu, aliokuwa akiwakata manyoya huko Karmeli. \v 3 Jina la mtu huyo lilikuwa Nabali, naye mkewe aliitwa Abigaili. Alikuwa mwanamke mwenye busara na mzuri wa sura, lakini mumewe, aliyekuwa wa ukoo wa Kalebu, alikuwa mwenye hasira na mchoyo katika utendaji wake. \p \v 4 Daudi alipokuwa huko jangwani, akasikia kuwa Nabali alikuwa anakata kondoo manyoya. \v 5 Basi akatuma vijana kumi na kuwaambia, “Pandeni kwa Nabali huko Karmeli, mkamsalimie kwa jina langu. \v 6 Mwambieni: ‘Amani iwe kwako! Amani iwe kwako pamoja na wa nyumbani mwako! Pia amani iwe pamoja na vyote ulivyo navyo! \p \v 7 “ ‘Nasikia kuwa huu ni wakati wa kukata kondoo manyoya. Wafugaji wako walipokuwa pamoja nasi, hatukuwatendea mabaya na wakati wote waliokuwa huko Karmeli hakuna chochote chao kilipotea. \v 8 Waulize watumishi wako nao watakuambia. Kwa hiyo uwatendee wema vijana wangu, kwani tumekuja wakati wa furaha. Tafadhali wape watumishi wako na mwanao Daudi chochote kitakachokuja mkononi mwako kwa ajili yao.’ ” \p \v 9 Watu wa Daudi walipofika wakampa Nabali ujumbe huu kwa jina la Daudi. Kisha wakangojea. \p \v 10 Nabali akawajibu watumishi wa Daudi, “Huyu Daudi ni nani? Huyu mwana wa Yese ni nani? Watumishi wengi wanakimbia kutoka kwa bwana zao siku hizi. \v 11 Kwa nini nichukue mkate wangu, maji yangu na nyama niliyochinja kwa ajili ya wakata manyoya wangu, na kuwapa watu ambao hakuna anayejua wanakotoka?” \p \v 12 Watu wa Daudi wakageuka na kurudi. Walipofika, wakaarifu kila neno. \v 13 Daudi akawaambia watu wake, “Jifungeni panga zenu!” Basi wakajifunga panga zao, naye Daudi akajifunga upanga wake. Watu kama mia nne hivi wakapanda pamoja na Daudi, na watu mia mbili wakabaki na vifaa. \p \v 14 Mmoja wa watumishi akamwambia Abigaili, mkewe Nabali: “Daudi alituma wajumbe kutoka jangwani kumpa bwana wetu salamu zake, lakini akawatukana. \v 15 Hata hivyo watu hawa walikuwa wema sana kwetu. Hawakututendea mabaya, na wakati wote tulipokuwa nje huko mashambani karibu nao, hatukupotewa na kitu chochote. \v 16 Usiku na mchana walikuwa ukuta wa ulinzi wakati wote tulipokuwa tukichunga kondoo wetu karibu nao. \v 17 Sasa fikiri juu ya jambo hili na uone unaweza kufanya nini, kwa sababu maafa yanakaribia juu ya bwana wetu na nyumba yake yote. Yeye ni mtu mwovu kiasi kwamba hakuna mtu awezaye kuzungumza naye.” \p \v 18 Abigaili akafanya haraka, akachukua mikate mia mbili, viriba viwili vya divai, kondoo watano waliochinjwa vipimo vitano vya bisi, vishada mia moja vya zabibu kavu, mikate mia mbili ya tini, akavipakia juu ya punda. \v 19 Kisha akawaambia watumishi wake, “Tangulieni; mimi nitakuja nyuma yenu.” Lakini hakumwambia Nabali mumewe. \p \v 20 Ikawa alipokuwa amepanda punda wake kwenye bonde la mlima, tazama, Daudi na watu wake wakawa wanateremka kumwelekea, naye akakutana nao. \v 21 Daudi alikuwa amesema, “Ilikuwa ni kazi bure kuchunga kwangu kote mali ya huyu mtu huko jangwani hivi kwamba hakuna chochote chake kilichopotea. Yeye amenilipa baya kwa ajili ya wema. \v 22 Mwenyezi Mungu na amwadhibu Daudi vikali zaidi, ikiwa kesho asubuhi nitambakizia mwanaume hata mmoja hai miongoni mwa watu wake wote!” \p \v 23 Abigaili alipomwona Daudi, akashuka haraka kwenye punda wake, akamsujudia Daudi. \v 24 Akamwangukia miguuni pake na kusema: “Bwana wangu, kosa hili na liwe juu yangu mwenyewe. Tafadhali mruhusu mtumishi wako aseme nawe. Sikia kile mtumishi wako atakachosema. \v 25 Bwana wangu na asimjali huyo mtu mwovu Nabali. Yeye anafanana na jina lake; jina lake ni Mpumbavu, nao upumbavu huenda pamoja naye. Lakini kwangu mimi, mtumishi wako, sikuwaona hao watu waliotumwa na bwana wangu. \p \v 26 “Basi sasa, bwana wangu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amekuzuia kumwaga damu na kulipiza kisasi kwa mikono yako mwenyewe, hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na kama uishivyo, adui zako na wote wanaokusudia kumdhuru bwana wangu wawe kama Nabali. \v 27 Nayo zawadi hii ambayo mtumishi wako amemletea bwana wangu, wapewe watu wanaofuatana nawe. \v 28 Tafadhali samehe kosa la mtumishi wako, kwa kuwa Mwenyezi Mungu kwa hakika ataifanya imara nyumba ya ufalme kwa bwana wangu, kwa sababu anapigana vita vya Mwenyezi Mungu. \v 29 Hata ingawa kuna mtu anayekufuatia ili akuue, usiruhusu baya lolote kuonekana kwako siku zote za maisha yako, uhai wa bwana wangu utafungwa salama kwenye furushi la walio hai na Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Lakini uhai wa adui zako utavurumishwa kama vile jiwe kutoka kombeo. \v 30 Mwenyezi Mungu atakapokuwa ameshamtendea bwana wangu kila kitu chema alichoahidi kumhusu na kumweka kuwa kiongozi wa Israeli, \v 31 bwana wangu hatakuwa na dhamiri inayolemewa na mzigo kwa kumwaga damu kusiko na sababu, au kujilipizia kisasi yeye mwenyewe. Mwenyezi Mungu atakapomletea bwana wangu mafanikio, umkumbuke mtumishi wako.” \p \v 32 Daudi akamwambia Abigaili, “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, aliyekutuma kunilaki leo. \v 33 Ubarikiwe kwa uamuzi wako mzuri na kwa kunizuia nisimwage damu leo na kulipiza kisasi kwa mikono yangu. \v 34 La sivyo, hakika kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye amenizuia nisiwadhuru, kama usingekuja haraka kunilaki, hakuna mwanaume hata mmoja wa Nabali angeachwa hai kufikia mapambazuko.” \p \v 35 Ndipo Daudi akapokea kutoka mkononi mwake kile alichokuwa amemletea, naye akasema, “Nenda nyumbani mwako kwa amani; nimesikia maneno yako na kukujalia ombi lako.” \p \v 36 Abigaili alipoenda kwa Nabali, alikuwa ndani ya nyumba yake akifanya karamu kama ile ya mfalme. Naye alikuwa ana furaha nyingi, akiwa amelewa sana. Kwa hiyo Abigaili hakumwambia mumewe kitu chochote hadi asubuhi yake. \v 37 Basi asubuhi, ulevi ulipokuwa umemtoka Nabali, mkewe akamwambia mambo yote, nao moyo wake ukazimia, akawa kama jiwe. \v 38 Baada ya siku kumi, Mwenyezi Mungu akampiga Nabali, naye akafa. \p \v 39 Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, akasema, “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, ambaye amenitetea dhidi ya Nabali kwa kuwa alinitendea kwa dharau. Amemzuia mtumishi wake asitende mabaya na Mwenyezi Mungu ameuleta ubaya wa Nabali juu ya kichwa chake mwenyewe.” \p Kisha Daudi akatuma ujumbe kwa Abigaili kumwomba awe mke wake. \v 40 Watumishi wa Daudi wakaenda Karmeli na kumwambia Abigaili, wakisema, “Daudi ametutuma kwako kukuchukua uwe mkewe.” \p \v 41 Akasujudu uso wake ukielekea chini, akasema, “Mjakazi wako yuko hapa, tayari kuwatumikia na kuwanawisha miguu watumishi wa bwana wangu.” \v 42 Abigaili akainuka kwa haraka, akapanda punda wake, akihudumiwa na wajakazi wake watano, akaenda pamoja na wajumbe wa Daudi, naye akawa mkewe. \v 43 Pia Daudi alikuwa amemwoa Ahinoamu wa Yezreeli, wote wawili wakawa wake zake. \v 44 Lakini Sauli alikuwa amemwoza Mikali binti yake, aliyekuwa mkewe Daudi, kwa Palti mwana wa Laishi, kutoka Galimu. \c 26 \s1 Daudi amwacha Sauli hai tena \p \v 1 Hao Wazifu wakamwendea Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kinachotazamana na Yeshimoni?” \p \v 2 Hivyo Sauli akashuka kwenda katika Jangwa la Zifu, akiwa na wapiganaji wake elfu tatu wa Israeli waliochaguliwa, ili kumtafuta Daudi huko. \v 3 Sauli akapiga kambi yake kando ya barabara juu ya kilima cha Hakila kinachotazamana na Yeshimoni, lakini Daudi alikuwa anaishi huko jangwani. Alipoona kuwa Sauli amemfuata huko, \v 4 Daudi akatuma wapelelezi na akapata habari kwa hakika kwamba Sauli alikuwa amewasili. \p \v 5 Ndipo Daudi akaondoka, akaenda hadi mahali ambapo Sauli alikuwa amepiga kambi. Akaona mahali Sauli na Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi, walipokuwa wamelala. Sauli alikuwa amelala ndani ya kambi, jeshi likiwa limemzunguka. \p \v 6 Basi Daudi akamuuliza Ahimeleki Mhiti, na Abishai mwana wa Seruya, nduguye Yoabu, akisema, “Ni nani atakayeshuka pamoja nami kambini kwa Sauli?” \p Abishai akajibu, “Nitaenda pamoja nawe.” \p \v 7 Hivyo Daudi na Abishai wakaenda kwenye jeshi wakati wa usiku, tazama Sauli, alikuwa amelala ndani ya kambi na mkuki wake umekitwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri na askari walikuwa wamelala kumzunguka Sauli. \p \v 8 Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Sasa niruhusu nimchome hadi ardhini kwa pigo moja la mkuki wangu; sitamchoma mara mbili.” \p \v 9 Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize! Ni nani awezaye kutia mkono juu ya mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu na asiwe na hatia?” \v 10 Daudi akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, Mwenyezi Mungu mwenyewe atampiga; au wakati wake utafika, naye atakufa, au ataenda vitani na kuangamia. \v 11 Lakini Mungu na apishie mbali nisije nikainua mkono juu ya mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu. Sasa chukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyo karibu na kichwa chake, tuondoke.” \p \v 12 Hivyo Daudi akachukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyokuwa karibu na kichwa cha Sauli, nao wakaondoka. Hakuna yeyote aliyeona au kufahamu habari hii, wala hakuna hata mmoja aliyeamka usingizini. Wote walikuwa wamelala, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amewatia kwenye usingizi mzito. \p \v 13 Kisha Daudi akavuka upande mwingine na kusimama juu ya kilima, mahali palipokuwa na nafasi pana kati yao. \v 14 Daudi akapaza sauti kwa jeshi na kwa Abneri mwana wa Neri, akisema, “Je, Abneri, hutanijibu?” \p Abneri akajibu, “Nani wewe unayemwita mfalme?” \p \v 15 Daudi akasema, “Wewe si ni mtu shujaa? Ni nani aliye kama wewe katika Israeli? Kwa nini basi hukumlinda mfalme bwana wako? Mtu mmoja alikuja kumwangamiza mfalme, bwana wako. \v 16 Ulichokifanya si kizuri. Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, wewe na watu wako mnastahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu. Tazameni hapo mlipo. Uko wapi mkuki wa mfalme na gudulia la maji ambavyo vilikuwa karibu na kichwa chake?” \p \v 17 Sauli akatambua sauti ya Daudi, na kusema, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” \p Daudi akajibu, “Naam, hiyo ndiyo, bwana wangu mfalme.” \v 18 Pia akaongeza, “Kwa nini bwana wangu anamfuatia mtumishi wake? Nimefanya nini, nalo kosa langu ni lipi nililolifanya niwe na hatia? \v 19 Sasa mfalme bwana wangu na asikilize maneno ya mtumishi wake. Kama Mwenyezi Mungu amekuchochea dhidi yangu, basi yeye na aipokee sadaka yangu. Lakini kama ni wanadamu waliofanya hivyo, walaaniwe mbele za Mwenyezi Mungu! Wao sasa wamenifukuza kutoka sehemu yangu katika urithi wa Mwenyezi Mungu wangu wakisema, ‘Nenda ukatumikie miungu mingine.’ \v 20 Basi usiache damu yangu imwagike kwenye ardhi mbali na uso wa Mwenyezi Mungu. Mfalme wa Israeli ametoka kutafuta kiroboto, kama vile mtu awindavyo kware katika milima.” \p \v 21 Ndipo Sauli akasema, “Nimetenda dhambi. Rudi, Daudi mwanangu. Kwa kuwa uliyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani leo, sitajaribu kukudhuru tena. Hakika nimetenda kama mpumbavu na nimekosa sana.” \p \v 22 Daudi akajibu, “Mkuki wa mfalme uko hapa. Mmoja wa vijana wako na avuke kuuchukua. \v 23 Mwenyezi Mungu humlipa kila mtu kwa ajili ya haki yake na uaminifu wake. Mwenyezi Mungu alikutia katika mikono yangu leo, lakini sikuinua mkono wangu juu ya mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu. \v 24 Kwa hakika kama vile maisha yako yalivyokuwa ya thamani kwangu leo, vivyo hivyo maisha yangu na yawe na thamani kwa Mwenyezi Mungu na kuniokoa kutoka taabu zote.” \p \v 25 Ndipo Sauli akamwambia Daudi, “Mwanangu Daudi na ubarikiwe; utafanya mambo makubwa na hakika utashinda.” \p Basi Daudi akaenda zake, naye Sauli akarudi nyumbani. \c 27 \s1 Daudi miongoni mwa Wafilisti \p \v 1 Daudi akasema moyoni mwake, “Katika mojawapo ya siku hizi nitaangamizwa kwa mkono wa Sauli. Jambo lililo bora ni kutorokea kwenye nchi ya Wafilisti. Hivyo Sauli atakata tamaa ya kunisaka popote katika Israeli, nami nitakuwa nimeponyoka mkononi mwake.” \p \v 2 Hivyo Daudi akaondoka na hao watu mia sita waliokuwa pamoja naye na kwenda kwa Akishi mwana wa Maoki mfalme wa Gathi. \v 3 Daudi na watu wake wakakaa huko Gathi pamoja na Akishi. Kila mtu alikuwa pamoja na jamaa yake, naye Daudi pamoja na wakeze wawili: yaani Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, mjane wa Nabali. \v 4 Sauli alipokuwa ameambiwa kwamba Daudi alikuwa amekimbilia Gathi, hakuendelea kumsaka tena. \p \v 5 Ndipo Daudi akamwambia Akishi, “Kama nimepata kibali machoni pako, unipe sehemu katika mojawapo ya miji katika nchi nikae huko. Kwa nini mtumwa wako akae pamoja nawe katika mji huu wa kifalme?” \p \v 6 Hivyo siku hiyo Akishi akampa Daudi mji wa Siklagi, nao Siklagi umekuwa mali ya wafalme wa Yuda tangu wakati huo. \v 7 Daudi akaishi katika nchi ya Wafilisti muda wa mwaka mmoja na miezi minne. \p \v 8 Basi Daudi na watu wake wakapanda na kuwashambulia Wageshuri, Wagirizi na Waamaleki. (Tangu zamani haya mataifa yalikuwa yameishi kwenye eneo lililotanda kuanzia Telemu katika njia iteremkayo Shuri hadi kufikia nchi ya Misri.) \v 9 Kila mara Daudi aliposhambulia eneo, hakubakiza hai mwanaume wala mwanamke, lakini alichukua kondoo na ng’ombe, punda na ngamia, na nguo. Kisha akarudi kwa Akishi. \p \v 10 Akishi alipomuuliza, “Je leo umeshambulia wapi?” Daudi humjibu, “Dhidi ya Negebu ya Yuda,” au wakati mwingine husema, “Dhidi ya Negebu ya Yerameeli,” au “Dhidi ya Negebu ya Wakeni.” \v 11 Daudi hakumwacha hai mwanaume au mwanamke ili apate kuletwa Gathi, kwa maana aliwaza, “Wanaweza kujulisha habari zetu na kusema, ‘Hivi ndivyo alivyofanya Daudi.’ ” Hii ndiyo ilikuwa desturi yake wakati wote aliishi katika nchi ya Wafilisti. \v 12 Akishi akamsadiki Daudi na kuwaza moyoni mwake, akasema, “Daudi amekuwa kitu cha kuchukiza kabisa kwa watu wake, Waisraeli, hivi kwamba atakuwa mtumishi wangu milele.” \c 28 \p \v 1 Siku zile Wafilisti wakakusanya majeshi yao ili kupigana vita dhidi ya Israeli. Akishi akamwambia Daudi, “Lazima ujue kuwa wewe pamoja na watu wako mtafuatana nami kwenda vitani.” \p \v 2 Daudi akasema, “Ndipo wewe mwenyewe utakapojionea jambo ambalo mtumishi wako anaweza kufanya.” \p Akishi akamjibu Daudi, “Vyema sana, mimi nitakufanya uwe mlinzi wangu daima.” \s1 Sauli na mchawi wa Endori \p \v 3 Wakati huo Samweli alikuwa amekufa, nao Waisraeli wote walikuwa wamemwombolezea na kumzika kwenye mji wake mwenyewe huko Rama. Sauli alikuwa amewafukuza waaguzi na wachawi. \p \v 4 Wafilisti wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu, naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao huko Gilboa. \v 5 Sauli alipoona jeshi la Wafilisti, akaogopa; moyo wake ukajawa na hofu kuu. \v 6 Ndipo Sauli akauliza ushauri kwa Mwenyezi Mungu, lakini Mwenyezi Mungu hakumjibu kwa ndoto, wala kwa Urimu\f + \fr 28:6 \fr*\ft Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha.\ft*\f*, wala kupitia manabii. \v 7 Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke mwaguzi ili nimwendee, nipate kuuliza kwake.” \p Watumishi wake wakamwambia, “Yuko mwanamke mmoja huko Endori.” \p \v 8 Hivyo Sauli akajigeuza kwa kuvaa mavazi mengine, naye usiku akiwa amefuatana na watu wawili wakaenda kwa huyo mwanamke. Akamwambia, “Nibashirie kwa uaguzi, unipandishie yule nitakayekutajia.” \p \v 9 Huyo mwanamke akamwambia, “Wewe unajua lile alilofanya Mfalme Sauli. Amewakatilia mbali waaguzi, wapiga ramli wote na wachawi katika nchi. Mbona umenitegea maisha yangu ili wapate kuniua?” \p \v 10 Sauli akamwapia huyo mwanamke kwa Jina la Mwenyezi Mungu, akasema, “Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, hutaadhibiwa kwa ajili ya jambo hili.” \p \v 11 Ndipo yule mwanamke akauliza, “Je unataka nikupandishie nani?” \p Sauli akasema, “Nipandishie Samweli.” \p \v 12 Yule mwanamke alipomwona Samweli, alipiga yowe kwa sauti kuu, naye akamuuliza Sauli, “Mbona umenidanganya? Wewe ndiwe Sauli.” \p \v 13 Mfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona nini?” \p Yule mwanamke akasema, “Naona mungu unapanda kutoka ardhini.” \p \v 14 Sauli akamuuliza, “Ni mfano wa nini?” \p Yule mwanamke akasema, “Ni mwanaume mzee amevaa joho anayepanda.” \p Ndipo Sauli akatambua kwamba ni Samweli. Sauli akasujudu, uso wake ukagusa chini. \p \v 15 Samweli akamuuliza Sauli, “Kwa nini unanitaabisha kwa kunipandisha juu?” \p Sauli akasema, “Mimi ninasumbuka sana, kwa maana Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, naye Mungu ameniacha. Hanijibu tena kupitia manabii wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita wewe ili unijulishe la kufanya.” \p \v 16 Samweli akamuuliza, “Kwa nini uniulize mimi, kuona Mwenyezi Mungu amekuacha na kuwa adui yako? \v 17 Mwenyezi Mungu ametenda lile alilotangulia kusema kupitia kwangu. Mwenyezi Mungu ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, naye amempa mmoja wa majirani zako, yaani Daudi. \v 18 Kwa sababu wewe hukumtii Mwenyezi Mungu, wala hukumtimizia ghadhabu yake kali juu ya Waamaleki, Mwenyezi Mungu amekutendea mambo haya leo. \v 19 Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu atawatia Israeli pamoja na wewe mikononi mwa Wafilisti, na kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. Mwenyezi Mungu pia atalitia jeshi la Israeli mikononi mwa Wafilisti.” \p \v 20 Papo hapo Sauli akaanguka chini, akajinyoosha, akiwa amejawa na hofu kwa ajili ya maneno ya Samweli. Nguvu zake zikamwishia kwa maana alikuwa hajala chochote mchana ule wote na usiku. \p \v 21 Yule mwanamke alipomwendea Sauli na kumwona amepatwa na hofu, akamwambia, “Tazama, mimi mtumishi wako mwanamke nimekutii. Nimeweka maisha yangu hatarini kwa kufanya kile ulichoniagiza nifanye. \v 22 Sasa tafadhali isikilize sauti ya mtumishi wako, uniruhusu nikupatie chakula kidogo ule ili uwe na nguvu za kurejea ulikotoka.” \p \v 23 Akakataa, akisema, “Mimi sitaki kula.” \p Lakini watumishi wake wakaungana na yule mwanamke wakamsihi ale, naye akakubali. Basi akainuka hapo chini, akaketi juu ya kitanda. \p \v 24 Yule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona hapo nyumbani, akamchinja mara moja. Akachukua unga, akaukanda, akatengeneza mkate usio chachu. \v 25 Ndipo akamwandalia meza Sauli pamoja na watu wake, nao wakala. Usiku ule ule wakainuka na kwenda zao. \c 29 \s1 Akishi amrudisha Daudi huko Siklagi \p \v 1 Wafilisti wakakusanya majeshi yao yote huko Afeki, nao Waisraeli wakapiga kambi karibu na chemchemi iliyo Yezreeli. \v 2 Watawala wa Wafilisti walipokuwa wakipita pamoja na vikosi vyao vya mamia na vya maelfu, Daudi na watu wake walikuwa wakitembea huko nyuma pamoja na Akishi. \v 3 Majemadari wa Wafilisti wakauliza, “Vipi kuhusu hawa Waebrania?” \p Akishi akajibu, “Huyu si Daudi, aliyekuwa afisa wa Sauli mfalme wa Israeli? Ameshakuwa pamoja nami kwa zaidi ya mwaka, naye tangu alipomwacha Sauli hadi sasa, sikuona kosa lolote kwake.” \p \v 4 Lakini majemadari wa Wafilisti wakamkasirikia na kusema, “Mrudishe mtu huyu, apate kurudi mahali pale ulipompangia. Haimpasi kufuatana pamoja nasi vitani, asije akageuka, akawa kinyume chetu vitani. Ni kwa njia ipi bora zaidi angeweza kujipatia tena kibali kwa bwana wake, isipokuwa kwa vichwa vya watu wetu wenyewe? \v 5 Je, huyu si ndiye Daudi walioimba kumhusu katika ngoma zao, wakisema: \q1 “ ‘Sauli amewaua elfu zake, \q2 naye Daudi makumi elfu yake’?” \p \v 6 Basi Akishi akamwita Daudi na kumwambia, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, wewe umekuwa mtu mwaminifu, nami ningependa utumike pamoja nami katika jeshi. Tangu siku ile uliyofika kwangu hadi sasa, sijaona kosa lolote kwako, lakini hao watawala hawakukubali. \v 7 Rudi na uende kwa amani; usifanye chochote cha kuwakasirisha watawala wa Wafilisti.” \p \v 8 Daudi akamuuliza Akishi, “Lakini mimi nimefanya nini? Je, umeona nini kibaya juu ya mtumishi wako tangu siku ile niliyokuja kwako hadi leo? Kwa nini nisirudi na kupigana na adui za bwana wangu mfalme?” \p \v 9 Akishi akamjibu Daudi, “Mimi ninajua ya kuwa wewe umekuwa wa kupendeza machoni pangu kama vile malaika wa Mungu. Lakini hao majemadari wa Wafilisti wamesema, ‘Huyu haimpasi kwenda vitani pamoja nasi.’ \v 10 Sasa amka mapema, pamoja na watumishi wa bwana wako waliofuatana nawe, nanyi ondokeni asubuhi mara kutakapopambazuka.” \p \v 11 Hivyo Daudi na watu wake wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda zao kurudi katika nchi ya Wafilisti, nao Wafilisti wakapanda kwenda Yezreeli. \c 30 \s1 Daudi aangamiza Waamaleki \p \v 1 Daudi na watu wake wakafika Siklagi siku ya tatu. Basi Waamaleki walikuwa wamevamia Negebu na Siklagi. Wakawa wameshambulia mji wa Siklagi na kuuteketeza kwa moto, \v 2 nao wakawa wamewachukua mateka wanawake pamoja na wote waliokuwamo humo, vijana na wazee. Hawakumuua yeyote, bali waliwachukua wakaenda zao. \p \v 3 Daudi na watu wake walipofika Siklagi, wakakuta mji umeangamizwa kwa moto na wake zao pamoja na wana wao wa kiume na wa kike wamechukuliwa mateka. \v 4 Hivyo Daudi na watu wake wakapaza sauti na kulia hadi wakaishiwa na nguvu za kulia. \v 5 Wake wawili wa Daudi walikuwa wametekwa: yaani Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli. \v 6 Daudi alihuzunika sana kwa sababu watu walikuwa wakisemezana kuhusu kumpiga kwa mawe. Kila mmoja alikuwa na uchungu rohoni kwa sababu ya wanawe wa kiume na wa kike. Lakini Daudi akajitia nguvu katika Mwenyezi Mungu, Mungu wake. \p \v 7 Kisha Daudi akamwambia kuhani Abiathari mwana wa Ahimeleki, “Niletee kizibau.” Abiathari akamletea, \v 8 naye Daudi akamuuliza Mwenyezi Mungu, “Je, nifuatie kundi hili la wavamizi? Je, nitawapata?” \p Mwenyezi Mungu akajibu, “Wafuatie. Hakika utawapata na utafanikiwa kuwaokoa.” \p \v 9 Daudi pamoja na watu wake mia sita wakafika kwenye Bonde la Besori, ambapo wengine waliachwa nyuma, \v 10 kwa kuwa watu mia mbili walikuwa wamechoka sana kuweza kuvuka hilo bonde. Lakini Daudi pamoja na watu mia nne wakaendelea kufuatia. \p \v 11 Wakamkuta Mmisri katika shamba fulani, nao wakamleta kwa Daudi. Wakampa huyo Mmisri maji ya kunywa na chakula; \v 12 kipande cha andazi la tini na andazi la zabibu zilizokaushwa. Akala naye akapata nguvu, kwa kuwa hakuwa amekula chakula chochote wala kunywa maji kwa siku tatu usiku na mchana. \p \v 13 Daudi akamuuliza, “Wewe ni wa nani, na umetoka wapi?” \p Akajibu, “Mimi ni Mmisri, mtumwa wa Mwamaleki. Bwana wangu alinitelekeza nilipougua siku tatu zilizopita. \v 14 Tulivamia Negebu ya Wakerethi, na nchi ya Yuda, na Negebu ya Kalebu. Nasi tulichoma moto Siklagi.” \p \v 15 Daudi akamuuliza, “Je, unaweza kuniongoza kufikia kundi hili la uvamizi?” \p Akajibu, “Niapie mbele ya Mungu kwamba hutaniua wala kunikabidhi mikononi mwa bwana wangu, nami nitakupeleka hadi waliko.” \p \v 16 Akamwongoza Daudi hadi mahali walipokuwa, nao walikuwa wametawanyika eneo lote, wakila, wakinywa na wakifanya karamu kwa sababu ya nyara nyingi walizochukua kutoka nchi ya Wafilisti na kutoka Yuda. \v 17 Daudi akapigana nao kuanzia machweo ya jua hadi kesho yake jioni, na hakuna yeyote miongoni mwao aliyetoroka, isipokuwa vijana mia nne waliopanda ngamia na kutoroka. \v 18 Daudi akarudisha kila kitu ambacho Waamaleki walikuwa wamechukua, pamoja na wake zake wawili. \v 19 Hakuna chochote kilichopotea: kijana au mzee, mvulana au msichana, nyara au kitu kingine chochote walichokuwa wamechukua. Daudi akarudisha kila kitu. \v 20 Akachukua makundi yote ya kondoo, mbuzi na ng’ombe, nao watu wake wakawaswaga wanyama hao mbele ya mifugo wengine, wakisema, “Hizi ni nyara za Daudi.” \p \v 21 Kisha Daudi akafika kwa wale watu mia mbili waliokuwa wamechoka sana kumfuata na ambao waliachwa nyuma kwenye Bonde la Besori. Wakatoka kwenda kumlaki Daudi na wale watu aliokuwa nao. Daudi na watu wake walipowakaribia, akawasalimu. \v 22 Lakini watu wote waovu na wakorofi miongoni mwa wafuasi wa Daudi wakasema, “Kwa sababu hawakuenda pamoja nasi, hatutagawana nao nyara tulizorudisha. Lakini, kila mtu aweza kuchukua mkewe na watoto wake na kuondoka.” \p \v 23 Daudi akajibu, “La, ndugu zangu, kamwe hamwezi kufanya hivyo kwa kile ambacho Mwenyezi Mungu ametupatia. Yeye ametulinda na kuweka mikononi mwetu majeshi yale yaliyokuja kupigana dhidi yetu. \v 24 Ni nani atasikiliza yale mnayosema? Fungu la mtu aliyekaa na vyombo litakuwa sawa na la yule aliyeenda vitani. Wote watashiriki sawa.” \v 25 Daudi akafanya hili liwe amri na agizo kwa Israeli kutoka siku ile hata leo. \p \v 26 Daudi alipofika Siklagi, akatuma baadhi ya nyara kwa wazee wa Yuda, waliokuwa rafiki zake, akasema, “Tazama, hapa kuna zawadi kwa ajili yenu kutoka nyara za adui za Mwenyezi Mungu.” \p \v 27 Akazituma kwa wale waliokuwa Betheli, Ramoth-Negebu na Yatiri; \v 28 kwa wale walio Aroeri, Sifmothi, Eshtemoa \v 29 na Rakali; kwa wale waliokuwa katika miji ya Wayerameeli na ya Wakeni; \v 30 na kwa wale walio Horma, Bori-Ashani, Athaki, \v 31 na kwa wakazi wa Hebroni; na kwa wale waliokuwa mahali pengine pote ambako Daudi na watu wake walitembelea. \c 31 \s1 Sauli ajiua \r (1 Nyakati 10:1-12) \p \v 1 Basi Wafilisti wakapigana na Israeli. Waisraeli wakawakimbia, na wengi wakauawa katika Mlima Gilboa. \v 2 Wafilisti wakawafuatilia Sauli na wanawe kwa karibu, na wakawaua Yonathani, Abinadabu, na Malki-Shua. \v 3 Mapigano yakawa makali sana dhidi ya Sauli, nao wapiga upinde wakampata na kumjeruhi vibaya. \p \v 4 Sauli akamwambia mbeba silaha wake, “Futa upanga wako unichome nao, la sivyo hawa watu wasiotahiriwa watakuja wanichome na kunidhalilisha.” \p Lakini mbeba silaha wake akaogopa sana wala hakuweza kufanya hivyo. Kwa hiyo Sauli akachukua upanga wake mwenyewe, akauangukia. \v 5 Mbeba silaha wake alipoona Sauli amekufa, pia akaangukia upanga wake, akafa pamoja naye. \v 6 Basi Sauli, wanawe watatu, mbeba silaha wake na watu wake wote wakafa pamoja siku ile ile. \p \v 7 Waisraeli waliokuwa kando ya bonde na wale waliokuwa ng’ambo ya Yordani walipoona kuwa jeshi la Waisraeli limekimbia na kwamba Sauli na wanawe wamekufa, wakaacha miji yao na kukimbia. Nao Wafilisti wakaenda na kukaa humo. \p \v 8 Kesho yake Wafilisti walipokuja kuwavua maiti silaha, walimkuta Sauli na wanawe watatu wameanguka katika Mlima Gilboa. \v 9 Wakamkata Sauli kichwa na kumvua silaha zake, nao wakatuma wajumbe katika nchi yote ya Wafilisti kutangaza habari katika hekalu la sanamu zao na miongoni mwa watu wao. \v 10 Wakaweka silaha zake katika hekalu la Maashtorethi, na kukifunga kiwiliwili chake katika ukuta wa Beth-Shani. \p \v 11 Watu wa Yabesh-Gileadi waliposikia yale Wafilisti waliyomfanyia Sauli, \v 12 mashujaa wao wote wakaenda usiku hadi Beth-Shani. Wakauchukua mwili wa Sauli na miili ya wanawe kutoka ukuta wa Beth-Shani na kurudi hadi Yabeshi, ambapo waliiteketeza miili kwa moto. \v 13 Kisha wakachukua mifupa yao na kuizika chini ya mti wa mkwaju huko Yabeshi, nao wakafunga kwa siku saba.